Oxfam yatahadharisha kuhusu madhara ya kuwazuia wahajiri kuingia Ulaya
Shirika la kimataifa la misaada ya kibinadamu la Oxfam lenye makao yake mjini London limeutahadharisha Umoja wa Ulaya kuhusu hatua yake ya kuwazuia wahajiri wanaotoka Libya kuingia barani humo.
Taarifa ya Oxfam imesema kuwa, hatua ya Umoja wa Ulaya ya kuwazuia wahajiri wa Libya kuingia barani Ulaya inawadhuru wanaume, wanawake na watoto wengi ambao hukabiliwa na udhalilishaji.
Taarifa ya Oxfam imesema kuwa wahajiri 158 waliohojiwa ambao sasa wamefika katika kisiwa cha Sicily nchini Italia wakitokea Libya wamesema kuwa, wanaishi katika mazingira magumu mno.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kambi zinazowahifadhi wakimbizi huko Italia zina hali mbaya na kwamba wahajiri waliopo kwenye kambi hizo wanakabiliwa na vitendo vya udhalilishaji, mateso na kulazimishwa kufanya kazi. Shirika hilo limesema kuwa, vitendo hivyo vyote vinashuhudiwa kila siku katika kambi za wakimbizi huko Italia.
Nchi za Ulaya katika miezi ya hivi karibuni zimechukua hatua kali na kuweka vizuizi mbalimbali lengo likiwa ni kuwazuia wahajiri kuingia barani humo, hatua ambayo imekabiliwa na upinzani wa mashirika na taasisi mbalimbali za kutetea haki za binadamu.