Watoto 34 waaga dunia hospitalini India kwa kukosa hewa
Watoto zaidi ya 30 wameripotiwa kupoteza maisha wakiwa katika hospitali moja ya serikali kaskazini mwa India, kwa kukosa hewa ya oksijeni ndani ya masaa 48.
Afisa wa polisi katika eneo hilo, Satyarth Aniruddha Pankaj amesema watoto 11 walifariki dunia jana Ijumaa, ikiwa ni chini ya masaa 24 baada ya wengine 23 kupoteza maisha hospitalini hapo kwa kosa oksijeni.
Habari zinasema kuwa, watoto hao walikuwa wamelazwa katika Hospitali ya Baba Raghav Das, kituo kiuu cha afya katika wilaya ya Gorakhpur, jimbo la kaskazini la Uttar Pradesh.
Duru za habari zimefichua kuwa, shirika lililokuwa likisambaza oksijeni katika hospitali hiyo lilikatiza huduma zake baada ya hospitali hiyo kushindwa kulipa madeni yake kwa kampuni hiyo.
Ashutosh Tandan, Waziri wa Huduma za Afya katika mkoa huo amedai kuwa hakuna vifo vilivyotokea katika hospitali hiyo kwa ukosefu wa hewa ya oksijeni.
Hata hivyo amesema amepokea agizo kutoka kwa Jaji wa Mahakama ya Wilaya ya Gorakhpur la kufanya uchunguzi mara moja juu ya kadhia hiyo na kuwasilisha ripoti kwake katika kipindi cha masaa 24 yajayo.