Trump, rais anayechukiwa zaidi katika historia ya Marekani
Rais Donald Trump wa Marekani ameshinda tuzo ya kuwa rais anayechukiwa zaidi katika historia ya nchi hiyo.
Uchunguzi wa maoni uliofanyika hivi karibuni umeonesha kuwa, kiwango cha kuchukiwa Donald Trump kinazidi kuongezeka nchini Marekani licha ya kupita miezi saba tu tangu kiongozi huyo ashike madaraka ya nchi.
Shirika la habari la Associated Press limeripoti kuwa, kiwango cha kupendwa na uungaji mkono wa Wamarekani kwa Rais Donald Trump wa nchi hiyo katika mwaka wa kwanza wa utawala wake kimekwenda chini ya kile cha marais wote waliowahi kuongoza nchi hiyo na kwenda chini ya asilimia 40.
Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa karibuni na taasisi ya Gallup yameonesha kuwa, asilimia 37 tu ya Wamarekani ndio wanaomuunga mkono Trump wakati wastani wa kiwango cha chini kabisa cha uungaji mkono wa Wamarekani kwa Barack Obama kilikuwa asilimia 40.
Mkurugenzi wa taasisi ya uchunguzi wa maoni ya Gallup, Frank Newport anasema: Marais wengi wa Marekani huanza kipindi cha utawala wao kwa fungate, na uungaji mkono wa wananchi hupungua kadiri miaka inavyosonga mbele, lakini Donald Trump hakuwa na fungate.
Uchunguzi wa maoni wa Gallup unaonesha kuwa, zaidi ya theluthi mbili ya watu wanaompinga na kumchukia Trump wanasema ni kutokana na shakhsia yake mbaya na hasi.