Daily Telegraph: Jeshi la Myanmar linawaua kwa umati Waislamu wa Rohingya
Gazeti la Daily Telegraph la nchini Uingereza limeandika katika ripoti yake kwamba, jeshi la Myanmar limekuwa likifanya mauaji ya umati dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya.
Gazeti hilo limeandika katika toleo lake la mtandaoni kwamba, kuna ushahidi unaoonyesha juu ya kuweko mauaji ya umati yanayofanywa na jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa Kirohingya.
Ripoti ya jarida la Daily Telegraph la Uingereza imeongeza kuwa, kuna mashuhuda waliohojiwa ambao wameeleza unyama na mauaji ya kutisha yanayofanywa na jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya ambao wamekuwa wakikabiliwa pia na hujuma na mashambulio ya Mabudha wenye misimamo ya kufurutu ada.
Mashuhuda hao wameelezea jinsi watoto wadogo wanavyouawa kwa kukatwa vichwa au watu kuchomwa moto wakiwa hai ambapo vitendo vyote hivyo vinafanywa na jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu hao wa Rohingya.
Ripoti hiyo imeongeza wasiwasi wa kushadidi maafa makubwa dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya katika jimbo la Rakhine.
Wakati huo huo, baadhi ya ripoti zinaonyesha kuwa, Waislamu takribani 400 wamefariki dunia nchini Myanmar katika kipindi cha wiki moja iliyopita tangu jeshi la nchi hiyo lianzishe kampeni mpya ya kuwakandamiza Waislamu wa jamii ya Rohingya.
Katika miaka ya karibuni, Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za Bangladesh, Thailand, Malaysia na Indonesia kutokana na mashambulio ya Mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka wanaoungwa mkono na serikali ya nchi hiyo.