UN kusaidia Waislamu Warohingya waliokimbia Myanmar
Idadi ya Waislamu wa jamii Warohingya ambao wanakimbia mateso na mauaji huko Myanmar inaongezeka kila uchao katika hali ambayo, mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wao wanaendelea kuhakikisha wanafikisha misaada ya dharura kwa wakimbizi hao ambao wengi wao ni Waislamu.
Habari zinasema kuwa, idadi ya wakimbizi hao walioingia Cox Bazar nchini Bangladesh tangu tarehe 25 mwezi uliopita imefikia zaidi ya 370,000 huku wakikabiliwa na safari ya vitisho na machungu.
Imeripotiwa kuwa, machungu hayo ni pamoja na serikali ya Myanmar kutandaza mabomu ya kutegwa ardhini kwenye mpaka wake na Bangladesh ili wananchi wanaokimbia washindwe kuvuka na wapoteze maisha kwa kuripukiwa na mabomu hata kabla ya kufika Bangladesh.
Adrian Edwards ambaye ni msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR mjini Geneva, Uswisi amesema, shehena ya zaidi ya tani 91 za misaada kama vile vifaa vya malazi iliwasili jana kwenye mji mkuu wa Bangladesh, Dhaka.
Nalo shirika la mpango wa chakula duniani, WFP linasema tayari liko Cox Bazar nchini Bangladesh likisambaza misada ambapo hofu yake kubwa ni afya ya wanawake na watoto wanaowasili wakiwa na njaa kali na utapiamlo uliokithiri.
Hayo yanajiri wakati ambapo mashirika ya kutetea haki za binadamu yamelikosoa vikali Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutokana na kutochukua msimamo imara mbele ya jinai zinazoendelea kufanywa na jeshi na Mabudha wa Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini humo.
Tangu Ijumaa ya tarehe 25 Agosti Waislamu wasiopungua elfu 6 na 334 wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar wameuwa na wengine zaidi ya elfu 8 kujeruhiwa katika wimbi jipya la mashambulizi na ukandamizaji unaofanywa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu katika mkoa wa Rakhine.