Misaada ya Iran yawafikia Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar
https://parstoday.ir/sw/news/world-i34501-misaada_ya_iran_yawafikia_waislamu_wa_rohingya_nchini_myanmar
Misaada ya dharura ya Iran imewafikia Waislamu wa jamii ya Rohingya waliokimbia mauaji ya kimbari nchini Myanmar na ambao wamepewa hifadhi nchini Bangladesh.
(last modified 2026-09-14T11:15:43+00:00 )
Sep 17, 2017 23:32 UTC
  • Misaada ya Iran yawafikia Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar

Misaada ya dharura ya Iran imewafikia Waislamu wa jamii ya Rohingya waliokimbia mauaji ya kimbari nchini Myanmar na ambao wamepewa hifadhi nchini Bangladesh.

Mkuu wa Hilali Nyekundu ya Iran ambaye anaogoza ujumbe wa timu ya wafanyakazi wa huduma za kibinadamu wa Iran amesema ndege yenye shehena ya misaada ya Iran imetua mjini Chittagong Bangladesh ikiwa na tani 40 za misaada ya dharura ya kibinadamu kwa ajili ya Waislamu wa jamii ya Rohingya. Amesema Iran itatuma tani zingine 160 za misaada hivi karibuni. Ndege hiyo ya misaada ya kibinadamu ya Iran ilikuwa na ujumbe wa ngazi za juu wa wataalamu wa kutoa misaada wakiwemo madaktari ambao watatathmini hali ya maskani, afya na chakula inayowakabili wakati huu Waislamu Warohingya walioko nchini Bangladesh.

Iran imekuwa mstari wa mbele katika kuwatetea Waislamu wa jamii ya Rohingya katika uga wa kimataifa huku viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakitaka nchi za Kiislamu zichukue hatua za kivitendo kuwasaidia Waislamu hao wanaoangamizwa kwa umati.

Maelfu ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wameuawa katika mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Jeshi la Myanmar na Mabuddha wenye misimamo ya kuchupa mipaka   

Wimbi jipya la mauaji ya Waislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa Myanmar lilianza tarehe 25 Agosti mwaka huu. Takribani Waislamu laki nne kutoka Myanmar wamekimbilia nchi ya Bangladesh na hali katika kambi za wakimbizi ni mbaya kutokana na kukosekana misaada ya kutosha.