Iran yatuma shehena ya pili ya misaada ya Waislamu Warohingya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i34651-iran_yatuma_shehena_ya_pili_ya_misaada_ya_waislamu_warohingya
Hilali Nyekundu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetuma shehena ya pili ya misaada ya dharura kwa ajili ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wanaopata hifadhi Bangladesh baada ya kukimbia mauaji ya kimbari katika nchi yao ya Myanmar.
(last modified 2026-08-17T09:53:57+00:00 )
Sep 21, 2017 03:08 UTC
  • Iran yatuma shehena ya pili ya misaada ya Waislamu Warohingya

Hilali Nyekundu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetuma shehena ya pili ya misaada ya dharura kwa ajili ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wanaopata hifadhi Bangladesh baada ya kukimbia mauaji ya kimbari katika nchi yao ya Myanmar.

Murtadha Salimi mkuu wa idara ya uokoaji katika Hilali Nyekundu ya Iran akizungumza na waandishi habari leo wakati wa kutumwa misaada hiyo amesema: "Msafara wa pili wa misaada ya kibinadamu ya Iran kwa ajili ya Waislamu Warohingya ina uzito wa tani 30 na inajumuisha mablanketi, mahema, vyakula, dawa na vifaa vya tiba."

Salimi ameongeza kuwa kabla ya kutumwa shehena mpya ya misaada, wataalamu wa Hilali Nyekundu ya Iran walitangulia kufika Bangladesh na kutathmini mahitaji ya Waislamu Warohingwa walio katika kambi za wakimbizi kusini magharibi mwa nchi hiyo katika mpaka na Myanmar. Wiki iliyopita Iran ilituma shehena ya kwanza ya misaada kwa ajili ya Waislamu wa Rohingya. Iran imesema itaendelea kutuma misaada zaidi kwa Waislamu hao wa Myanmar wanaokabiliwa na mauaji ya umati.

Waislamu wa jamii wa Rohingya

Maelfu ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wameuawa katika mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Jeshi la Myanmar na Mabuddha wenye misimamo ya kuchupa mipaka   

Wimbi jipya la mauaji ya Waislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa Myanmar lilianza tarehe 25 Agosti mwaka huu. Takribani Waislamu laki nne kutoka Myanmar wamekimbilia nchi ya Bangladesh na hali katika kambi za wakimbizi ni mbaya kutokana na kukosekana misaada ya kutosha.