Wamarekani waendelea kukosoa hotuba ya Trump katika UN
Viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa wameendelea kukosoa vikali hotuba na matamshi yaliyotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani katika mkutano wa 72 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.
Naibu Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani, Nicholas Burns amesema kuwa, Trump anapaswa kutofautisha baina ya hotuba anazotoa kwa mashabiki na waungaji mkono wake ndani ya Marekani na zile anazotoa katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Burns amekosoa matamshi makali ya Donald Trump dhidi ya Iran na kusema kuwa, kujiondoa kwa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya nchi wanachama wa kundi la 5+1 na Iran kwa kifupi JCPOA itakuwa hatua isiyo sahihi na kudai kuwa: Iran imeondokana na vikwazo vya kimataifa na iwapo Marekani itajiondoa katika makubaliano ya JCPOA vizuizi vyote vya miradi ya nyuklia ya Iran vitaondoka.
Katika hotuba yake kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais Donald Trump wa Marekani amedai kuwa makubaliano ya nyuklia ya Iran na nchi wanachama katika kundi la 5+1 ndiyo mabaya zaidi yaliyowahi kusainiwa na Marekani.
Matamshi makali ya Trump dhidi ya Iran na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yamekosolewa vikali ndani na nje ya nchi hiyo.
Wakati huo huo mshauri wa zamani wa usalama wa taifa wa Marekani, Susan Rice amesema hotuba ya Donald Trump katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa haikustahili kusemwa na ilichupa mipaka kupita kiasi.
Rice ambaye pia aliwahi kuwa mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, maneno ya vitisho na kutishia kuangamiza kabisa taifa la nchi nyingine si njia inayofaa ya kutatua matatizo ya kimataifa.
Katika hotuba yake ya juzi pia Trump alisema kuwa, ataiangamiza kikamilifu nchi ya Korea Kaskazini.