Zarif: Iran itaendelea kuwa pamoja na Wasyria kujenga upya nchi yao
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Javad Zarif amesema kuwa Tehran inaunga mkono uzingatiaji wa kimataifa juu ya umuhimu wa kuendelea kutolewa misaada ya kibinaadamu na ukarabati wa Syria na kwamba katika hilo Iran itaendelea kushirikiana na Wasyria katika kuijenga upya nchi yao.
Zarif ameyasema hayo baada ya kumalizika kikao maalumu cha Umoja wa Mataifa juu ya mustakbali wa Syria kilichofanyika katika ofisi za umoja huo mjini New Yok, Marekani na kuongeza kuwa kutolewa misaada ya kibinaadamu kwa ajili ya Syria na kadhalika kujengwa upya nchi hiyo ya Kiarabu ni harakati chanya hasa kwa kuzingatia kuwa katika miezi ya hivi karibuni muqawama dhidi ya makundi ya kigaidi na ukufurishaji hususan Daesh (ISIS) umekuwa na mafanikio makubwa nchini humo.
Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hadi sasa maeneo mengi ya Syria yamekombolewa na kurejea mikononi mwa udhibiti wa serikali ya Damascus. Akiashiria kwamba idadi kubwa ya Wasyria waliokuwa wamekimbia nchi yao kutokana na vita sasa wanarejea makwao amesema kuwa, kwa kuzingatia suala hilo kuna udharura wa kufikiriwa njia za kurejesha usalama wa kisiasa na kuijenga upya nchi hiyo. Mohammad Javad Zarif amesisitiza kuwa, hatua ya jamii ya kimataifa kuhisi majukumu yake juu ya kutolewa misaada zaidi ya kibinaadamu kwa sharti la kujitenga mbali na malengo ya kisiasa, ni yenye kupongezwa na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuzingatia juhudi kubwa zilizofanyika za ufikishaji misaada hiyo katika miaka iliyopita, itaendelea kuwa pamoja na raia wa taifa hilo katika kulijenga upya taifa lao. Kikao maalumu kuhusiana na Syria kilifanyika jana Alkhamisi mjini New York pembeni ya mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).