Russia: Marekani haiwezi kuthubutu kuishambulia Korea Kaskazini
https://parstoday.ir/sw/news/world-i34803-russia_marekani_haiwezi_kuthubutu_kuishambulia_korea_kaskazini
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa, Marekani haithubutu kufanya shambulizi lolote dhidi ya Korea Kaskazini kwa kuwa inafahamu fika kwamba Pyongyang ina mabomu ya nyuklia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 25, 2017 04:09 UTC
  • Russia: Marekani haiwezi kuthubutu kuishambulia Korea Kaskazini

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa, Marekani haithubutu kufanya shambulizi lolote dhidi ya Korea Kaskazini kwa kuwa inafahamu fika kwamba Pyongyang ina mabomu ya nyuklia.

Katika mahojiano na kanali ya televisheni ya NTV ya Russia jana Jumapili, Sergei Lavrov alisema kama tunavyomnukuu: "Marekani iliishambulia kijeshi Iraq kwa kuwa ilijua kuwa nchi hiyo ya Kiarabu haina silaha za maangamizi, lakini haiwezi kuishambulia Korea Kaskazini wakati ambapo ina uhakika kuwa nchi hiyo ina silaha za nyuklia."

Kadhalika Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia ameyataja malumbano kati ya Donald Trump wa Marekani na Kim Jong-un wa Korea Kaskazini kama 'malumbano ya chekechea' kati ya watoto wadogo.

Trump (Kushoto) na Kim Jong-un

Akiongea hivi karibuni katika Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Trump alisema ikibidi Marekani itaiangamiza kikamilifu nchi hiyo ya Asia isipoachana na miradi yake ya silaha za nyuklia. 

Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini alijibu matamshi ya vitisho ya Trump na kusema kuwa, rais huyo wa Marekani ana matatizo ya kiakili na kwamba atalipa gharama ya matamshi yake ya uhasama dhidi ya Pyongyang.

Pyongyang imekuwa ikisisitiza kuwa, itaendelea kujiimarisha kijeshi ili kukabiliana na chokochoko za Marekani na washirika wake dhidi yake.