Mamilioni ya Waislamu duniani katika maombolezo ya Ashura
https://parstoday.ir/sw/news/world-i35083-mamilioni_ya_waislamu_duniani_katika_maombolezo_ya_ashura
Mamilioni ya Waislamu kote duniani leo wanashiriki katika maombolezo ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Hussein AS katika siku ya Ashura.
(last modified 2024-06-10T09:25:34+00:00 )
Oct 01, 2017 07:55 UTC
  • Maandamano ya Ashura leo mjini Dar es Salam nchini Tanzania
    Maandamano ya Ashura leo mjini Dar es Salam nchini Tanzania

Mamilioni ya Waislamu kote duniani leo wanashiriki katika maombolezo ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Hussein AS katika siku ya Ashura.

Itakumbukwa kuwa, siku kama ya leo miaka 1378 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Kiislamu na ya mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na batili katika ardhi ya Karbala huko Iraq.

Siku hii inajulikana kwa jina la Ashura. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume SAW, Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi kubwa la batili ili kuilinda dini ya Allah. Katika kukumbuka siku hiyo, Waislamu huomboleza katika siku 10 za mwezi wa Muharram na kilele chake huwa ni siku ya 10 ambayo ni maarufu kama Ashura.

Imam Hussein AS alitangaza wazi kwamba lengo lake la kuanzisha mapambano hayo lilikuwa ni kuamrisha mema na kukataza mabaya pamoja na kuhuisha mafundisho na thamani za dini ya Mtume Mtukufu SAW.

Karbala, Iraq katika Siku ya Ashura

Hapa nchini Iran mamilioni ya waumini wameshiriki katika maomboolezo yanayoendelea katika mitaa na medani mbali mbali huku kilele cha maombolezo hayo kikiwa ni Sala ya Jamaa ya Adhuri ya siku hii ya Ashura. Aidha katika maeneo mengine duniani Waislamu wameshiriki katika maombolezo ya Ashura ambapo leo katika mji wa Dar es Salaam nchini Tanzania Waislamu wamefanya matembezi kwa munasaba wa Siku ya Ashura.

Aidha katika mji wa Karbala Iraq, iliko Haram Takatifu ya Imam Hussein AS, kuna mjumuiko mkubwa wa aina yake wa mamilioni ya waumini wanaohuisha siku hii adhimu.