Azerbaijan yapiga marufuku watoto kushiriki hafla za Kiislamu
Katika kile kinachoonekana ni mwendelezo wa ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia, serikali ya Azerbaijan inatazamiwa kupasisha sheria inayopiga marufuku watoto kushiriki katika hafla na sherehe za kidini.
Kamati ya Masuala ya Familia, Wanawake na Watoto ambayo ipo chini ya Baraza la Mawaziri imetoa taarifa inayosema kuwa, iwapo pendekezo lake litaidhinishwa na Bunge la nchi hiyo, basi watoto watapigwa marufuku kushiriki katika sherehe za kidini yakiwemo matembezi ya Muharram.
Kamati hiyo imedai kuwa, lengo la muswada huo ni kuwakinga watoto kutokana na 'Taarifa zenye madhara kwa Afya na Malezi yao'.
Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya Azerbaijan kwa kushirikiana na Bunge la nchi hiyo imezidisha hatua za ukandamizaji dhidi ya Waislamu hususan wa madhehebu ya Shia ambao wanaunda asilimia kubwa ya wananchi wa taifa hilo la Asia Magharibi.

Kwa mujibu wa sheria zilizowekwa na serikali ya mji mkuu wa nchi hiyo Baku, ni makosa wasomi waliosomea katika baadhi ya nchi za Kiislamu kama Iran kusalisha Swala za jamaa mjini hapo.
Itakumbukwa kuwa, mwaka 2015, Waislamu watano wa Kishia waliuawa huku makumi ya wengine wakitiwa mbaroni na maafisa usalama wa Azerbaijan katika mji wa Nardaran, wakati wa shughuli ya Arubaini ya Imam Hussein AS.