Oct 11, 2017 08:17 UTC
  • 17 wapoteza maisha baada ya moto kuteketeza misitu, makazi Marekani

Watu wasiopungua 17 wamefariki dunia katika mkasa wa moto unaoendelea kuteketeza misitu katika jimbo la California nchini Marekani.

Kadhalika watu 180 wameripotiwa kutoweka kutokana na mkasa huo, ambao haujasaza majengo mbali na kuathiri pakubwa suhula za mawasiliano.

Habari zinasema kuwa, moto huo ambao umetekeketeza zaidi ya ekari 115,000 za ardhi umesababisha watu zaidi ya elfu 20 kukimbia makazi yao katika maeneo kadhaa ya jimbo hilo.

Vyombo vya habari nchini Marekani vimeripoti kuwa, moto mkubwa zaidi umeshuhudiwa katika maeneo ya Napa na Mendocino, huku ardhi yenye ukubwa wa ekari 52,000 ikiteketea moto katika maeneo ya Sonoma, Napa, Tubbs na Atlas.

Afisa wa zimamoto kazini, jimboni California

Sajenti wa kaunti ya Sonoma, Spencer Crum amesema upepo mkali unaokwenda kwa kasi ya mita 60 kwa saa umesababisha moto huo kuenea kwa kasi, ambapo wakazi elfu tatu wameathiriwa, huku nyumba elfu 2 zikiteketea.

Haya yanajiri siku chache baada ya kimbunga cha Irma kuua watu wasiopungua 22 nchini Marekani, ambapo makumi ya mamilioni ya wengine walibaki bila umeme kufuatia janga hilo. Kimbunga hicho kiliibuka wiki mbili baada ya kile cha Harvey kusababisha mafuriko makubwa nchini humo na kuuwa watu karibu 70. 

Tags