Umoja wa Ulaya wasisitiza utekelezwaji kikamilifu mapatano ya nyuklia ya Iran
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya Jumatatu baada ya kumalizika kikao chao mjini Luxembourg walitoa taarifa na kutuangaza kuunga mkono na kuendeleza ushirikiano kuhusu mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji, JCPOA.
Msimamo wa Umoja wa Ulaya kuhusu mapatano hayo umetokana na msingi wa kuunga mkono maafikiano yaliyofikiwa kwa mujibu wa taratibu za kimataifa.
Taarifa hiyo imetangaza kuunga mkono mapatano hayo ambayo Umoja wa Ulaya ulikuwa miongoni mwa watiaji saini wake. Itakumbukwa kuwa Umoja wa Ulaya ulikuwa unasimamia mazungumzo ya nyuklia baina ya Iran na nchi za 5+1 ambazo ni Russia, China, Ufaransa, Uingereza, Marekani pamoja na Ujerumani. Nchi hizo zilifikia mapatano ya nyuklia na Iran Julai mwaka 2015. Katika taarifa, Umoja wa Ulaya umesema: "JCPOA ni kilele cha miaka 12 ya ushirikiano wa kidiplomasia barani Ulaya na mapatano hayo yaliidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitia azimio 2231."
Kwa mtazamo wa Umoja wa Ulaya, uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekani wa kutoidhinisha kufungamana Iran na mapatano hayo ni suala la ndani ya Marekani. Ni wazi kuwa Umoja wa Ulaya hautaki kukosa kunufaika na mapatano ya JCPOA kwa sababu ya misuguano ya kisiasa na Marekani.
Taarifa hiyo ya Umoja wa Ualya inaitaka Marekani ifungamane na mapatano hayo ya kimataifa. Mtandao wa uchambuzi wa sera za kigeni wa LobeLog umeandika hivi kuhusu kadhia hiyo: "Umoja wa Ulaya ni mtetezi imara wa JCPOA na umoja huo hautaki kusalimu amri mbele ya matakwa ya Marekani."
Weledi wengi wa mambo wanasema Umoja wa Ulaya hautaki kupoteza fursa zinazotokana na mapatano ya nyuklia ya Iran.
Lakini pamoja na hayo, kama ambavyo ilitabiriwa, Umoja wa Ulaya umekariri tena madai yake dhidi ya Iran. Sehemu ya taarifa hiyo ya kikao cha Luxembourg imesema umoja huo una wasiwasi kuhusu uwezo wa Iran katika makombora ya balistiki na pia kile kinachotajwa kuwa eti ni Iran kuhusika na ongezeko la misiguano katika eneo la Mashariki ya Kati. Taarifa hiyo hata hivyo imesema maudhui hizo zinapaswa kuchnguzwa nje ya fremu ya mapatano ya JCPOA.
Kilicho wazi ni kuwa Umoja wa Ulaya hauoni maslahi yaoyote katika kufuata msimamo wa Marekani kuhusu JCPOA na hivyo unajaribu kulinda ahadi na itibari yake kimataifa.
Hakuna shaka kuwa Marekani itapinga msimamo huo na jambo hilo litauweka Umoja wa Ulaya katika hali ngumu sana. Hapa Umoja wa Ulaya hautakuwa na budi ila kuchagua moja ya njia mbili; ima kuchukua hatua ya mkondo wa maamuzi huru na hivyo kuimarisha itibari na hadhi yake kimataifa au kusalimu amri mbele ya mashinikizo ya Marekani na ikichagua njia hiyo ya pili hilo halitaishia tu katika JCPOA bali katika masuala mengine na hivyo kuudhuru umoja huo.
Tarifa ya kikao cha Luxembourg inaonyesha kuwa Umoja wa Ulaya unakusudia kutetea haki za umoja huo na JCPOA ni kati ya haki hizo. Pamoja na hayo tunapaswa kusubiri kuona katika siku chache zijazo mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini atachukua muelekeo upi kuhusu Marekani. Hii ni kwa sababu anatazamiwa kuelekea Washington kukutana na wakuu wa nchi hiyo pamoja na Bunge la Kongresi mwanzoni mwa mwezi Novemba.