Korea Kusini yatishia kuangamiza silaha zote za Korea Kaskazini
Jeshi la Korea Kusini limetoa vitisho vikali ambavyo havijazoeleka kwa kudai kuwa ikiwa kutaibuka vita na mapigano katika eneo hilo, basi litaangamiza makombora yote ya balestiki ya Korea Kaskazini.
Taarifa iliyotolewa na jeshi la Korea Kusini imesisitiza kuwa, ikiwa vita katika eneo la Peninsula ya Korea vitaibuka, basi nchi hiyo itafanya haraka sana kwa kutumia makombora na uwezo wake mkubwa wa kijeshi kusambaratisha silaha za nyuklia na makombora ya balestiki ya nchi hiyo jirani yake.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, hatua ya Marekani ya kupeleka katika Peninsula ya Korea zana za silaha za nyuklia na kadhalika kuendesha maneva ya kijeshi ya wiki moja kwa kushirikiana na Korea Kusini imetajwa na Pyongyang kuwa hatari sana na ambayo inaweza kuibua vita vya nyuklia wakati wowote ule.
Kadhalika Korea Kaskazini imetishia kutekeleza mashambulizi ya kushtukiza na yasiyotarajiwa dhidi ya Marekani kutokana na chokochoko zake dhidi ya Pyongyang.
Korea Kaskazini imekuwa ikisisitiza kuwa itaendelea kujizatiti kwa silaha za nyuklia na makombora ya balestiki maadamu Marekani ingali inaendeleza chokochoko zake dhidi yake katika eneo.
Hadi sasa Marekani imetuma meli kadhaa za kubeba ndege za kivita na ndege za kivita zenye uwezo mkubwa wa kushambulia kwa mabomu kwenda bahari ya Pacific na Peninsula ya Korea kwa wenzo wa kukabiliana na Korea Kaskazini, hatua ambayo imetajwa na weledi wengi wa masuala ya kisiasa kuwa ni hatua za uchokozi.