Myanmar yakosoa mpango wa Seneti ya US kuiwekea vikwazo vya kijeshi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i36144-myanmar_yakosoa_mpango_wa_seneti_ya_us_kuiwekea_vikwazo_vya_kijeshi
Serikali ya Myanmar imeonya kuwa, kutakuweko na taathira hasi iwapo Bunge la Seneti la Marekani litapasisha muswada wa kuiwekea nchi hiyo vikwazo vya kijeshi.
(last modified 2026-02-22T02:21:18+00:00 )
Nov 04, 2017 02:40 UTC
  • Myanmar yakosoa mpango wa Seneti ya US kuiwekea vikwazo vya kijeshi

Serikali ya Myanmar imeonya kuwa, kutakuweko na taathira hasi iwapo Bunge la Seneti la Marekani litapasisha muswada wa kuiwekea nchi hiyo vikwazo vya kijeshi.

Zaw Htay, msemaji wa Aung San Suu Kyi, Waziri wa Mambo ya Nje na Mashauri Mkuu wa nchi hiyo amesema nchi hiyo inahitaji uthabiti na kuiwekea vikwazo vya kijeshi wakati huu kutayumbisha uwekezaji na safari za raia wa kawaida na wala sio wanajeshi tu.

Amesema jeshi la nchi hiyo linalofahamika kama Tatmadaw sharti lihusishwe katika mchakato wa kipindi cha mpito nchini humo, na kuliwekea vikwazo kutakuwa na madhara makubwa.

Hii ni katika hali ambayo, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) mapema mwezi jana lilisema jeshi la Myanmar linawaua kiholela na kuwanajisi Waislamu wa jamii ya Rohingya magharibi mwa nchi hiyo.

Silaha zilizoundwa nchini Marekani

Hivi karibuni, Walter Lohman, Mkurugenzi wa Mipango barani Asia wa shirika la kutetea haki za binadamu la Heritage Foundation alikosoa vikali muswada uliowasilishwa katika Kongresi ya Marekani wa kutaka kuimarishwa uhusiano wa kijeshi kati ya Marekani na Myanmar. Alisisitiza kuwa: "Kuimarishwa uhusiano wa moja kwa moja wa kijeshi na Burma wakati huu ni jambo ambalo haliingii akilini, hatua hiyo inatuma ujumbe wa kuogofya kwa dunia."

Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi nchi hiyo tangu tarehe 25 Agosti mwaka huu hadi sasa.