Akthari ya watu wa bara la Ulaya wanamchukia Trump
Uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa unaonyesha kuwa akthari ya watu katika nchi za Ulaya wanamchukia Rais wa Marekani Donald Trump.
Kwa mujibu wa gazeti la Kifaransa la L'Express, matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na taasisi ya utafiti ya Odoxa kuhusu Rais Donald Trump wa Marekani barani Ulaya umeonyesha kuwa kwa wastani, asilimia 85 ya raia wa nchi za bara hilo wanamchukia kiongozi huyo.
Matoko ya uchunguzi huo uliofanywa na taasisi ya Odoxa yanaonyesha kuwa hivi sasa Trump ni mtu asiyependeza mbele ya asilimia 85 ya raia wa nchi za Ulaya ilhali kiwango cha chuki dhidi ya kiongozi huyo katika uchunguzi wa maoni uliofanywa mwezi Januari mwaka huu kilikuwa ni asilimia 75 kikiwa ni cha chini zaidi kulinganisha na sasa kwa asilimia 10.
Asilimia 81 ya Wafaransa walioshiriki kwenye uchunguzi huo wa maoni wamemzungumzia Trump kuwa ni mtu "hatari".
Taasisi ya Odoxa imefafanua kuwa asilimia 90 ya Wajerumani wanamchukia rais huyo wa Marekani huku asilimia 92 ya raia wa Uhispania nao pia wakiwa hawapendezwi na kiongozi huyo.
Kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi huo wa maoni, nchini Italia pia asilimia 76 ya raia wa nchi hiyo waliotoa maoni yao, wanamchukia rais huyo wa Marekani ambaye ana kiwango cha chini cha umaarufu pia hata ndani ya nchi yake.../