Radiamali ya OIC kwa siasa za Rais Trump kuhusiana na Quds
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC imemtahadharisha Rais Donald Trump wa Marekani kuhusiana na kuutambua mji wa Quds kama mji mkuu wa utawala haramu wa Israel.
Taarifa ya OIC iliyotolewa siku ya Jumatatu imeeleza kwamba, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu inatambua hatua ya kuuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuupeleka Baytul Muqaddas kuwa, ni 'uvamizi wa wazi' dhidi ya nchi za Kiislamu. Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC imesisitiza kwamba, nchi zote wanachama wa jumuiya hiyo zinapaswa kukata uhusiano na nchi yoyote ambayo inahamishia ubalozi wake huko Baytul Muuqaddas.
Wiki iliyopita, Mike Pence, Makamu wa Rais wa Marekani alitangaza kuwa, kuna uwezekano katika siku chache zijazo Rais Trump akaafiki suala la kuhamishiwa ubalozi wa Washington huko Baytul Muqaddas na anatarajiwa pia kuutambua rasmi mji wa Baytul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Hii ni katika hali ambayo, katika radiamali yake ya jana Jumatatu kuhusiana na ukosoaji wa kimataifa kuhusiana na hatua hiyo, White House ilitangaza kuwa, bado Rais Trump hajafikia uamuzi wa mwisho kuhusu suala la kuuhamisha ubalozi wa nchi hiyo kutoka Tel Aviv na kuupeleka Baytul Muqaddas. Aidha baadhi ya duru zimefichua kwamba, Rais Trump ameakhirisha uamuzi wake kuhusiana na kadhia hiyo.
Ubadilishaji huo wa uamuzi ambao kwa kiwango fulani unahesabiwa kuwa, ni kulegeza kamba viongozi wa Marekani unafanyika katika hali ambayo, wakati wa kampeni za uchaguzi wa Marekani Donald Trump alitangaza mara kadhaa kwamba, angeuhamishia Baytul Muqaddas ubalozi wa nchi yake ulioko huko Tel Aviv. Aidha alimuahidi mara kadhaa Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel kwamba, atatekeleza uamuzi wake huo.
Hatua ya Trump ya kung'ang'ania kutaka kuhamishia ubalozi wa Marekani huko Baytul Muqaddas imemgeuza Rais huyo wa 45 wa Marekani kuwa kiongozi anayependwa zaidi na Wazayuni. Hatua hiyo ambayo ilikuwa ikihesabiwa kuwa moja ya nara za Donald Trumop katika kampeni zake za uchaguzi wa Rais, kuanzia Januari mwaka huu baada ya kiongozi huyo kuapishwa na kushika hatamu za uongozi wa White House, aliamua kuliweka hilo katika ajenda zake za siasa za kgieni.
Hata hivyo kila mara uamuzi huo haukutekelezwa kivitendo kutokana na sababu mbalimbali. Suala la kuhamishiwa ubalozi wa Marekani huko Baytul Muqaddas lilipasishwa mwaka 1995 katika Kongresi ya Marekani.
Katika miaka hii yote serikali zilizotangulia za Bill Clinton, George Bush na Barack Obama ziliakhirisha kutekeleza uamuzi huo kutokana na woga wa radiamali ya kimataifa na matokeo mabaya ya kidiplomasia ambayo yanaweza kuwa na madhara kwa Marekani. Hapana shaka kuwa, endapo Trump atafanya makosa na kuutekeleza kivitendo uamuzi wake huo usio wa busara, bila shaka matokeo yake yatakuwa mabaya kwa Marekani. Hata kama hadi sasa haijafahamika wazi uamuzi wa mwisho wa Trump kuhusiana na suala hilo, lakini tayari radiamali na malalamiko yanaonekana kuongezeka katika kila kona ya dunia.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepasisha kwa wingi wa kura azimio ambalo linaiarifisha Israel kwamba, ni utawala vamizi huko Baytul Muqaddas. Kwa muujibu wa azimio hilo Israel haina uhusiano wa aina yoyote ile na mji huo na kwamba, hatua yoyote inayochukuliwa na Israel ya kutwisha sheria katika mji huo ni batili na isiyokubalika.
Kwa kuzingatia unyeti maalumu wa kadhia ya Quuds kwa Wapalestina na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla na fikra za waliowengi ulimwenguni, hapana shaka kuwa, hatua yoyote ile ya Marekani ya kufuata siasa za kupenda kujitanua Israel huko Quds itaigharimu pakubwa Washington kisiasa, kiuchumi na hata kidiplomasia.