Trump, White House watengwa kutokana na uamuzi dhidi ya Quds
https://parstoday.ir/sw/news/world-i37503-trump_white_house_watengwa_kutokana_na_uamuzi_dhidi_ya_quds
Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon amesema kitendo cha Donald Trump cha kuitangaza Quds ambayo ina Kibla cha Kwanza cha Waislamu kuwa eti ni mji mkuu wa Israel imeifanya Ikulu ya White House na rais huyo wa Marekani watengwe kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 12, 2017 04:47 UTC
  • Trump, White House watengwa kutokana na uamuzi dhidi ya Quds

Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon amesema kitendo cha Donald Trump cha kuitangaza Quds ambayo ina Kibla cha Kwanza cha Waislamu kuwa eti ni mji mkuu wa Israel imeifanya Ikulu ya White House na rais huyo wa Marekani watengwe kimataifa.

Akihutubia taifa kutoka eneo la Dahieh, viungani mwa mji mkuu Beirut jana Jumatatu, Sayyid Hassan Nasrullah ameshukuru nchi, taasisi na wapenda haki kote duniani waliopaza sauti kulaani chokochoko hizo mpya za Marekani, na kuonyesha uungaji mkono wao kwa harakati ya muqawama.

Sayyid Nasrullah amesema maamuzi yote yaliyotolewa na Trump dhidi ya Quds tukufu ni hasi na yamesababisha nchi hiyo kuendelea kutengwa kimataifa.

Mbali na kuashiria kuhusu maandamano ya kulaani kitendo hicho cha Trump katika pembe zote za dunia, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ametoa mwito wa kutumia majukwaa mbalimbali kama vile mitandao ya kijamii kuendeleza wimbi hilo la kuilaani Marekani kutokana na kitendo chake cha kihasama na kichokozi dhidi ya ulimwengu wa Kiislamu.

Waandamanaji katika kila kona ya dunia wamekuwa wakiteketeza moto bendera ya Israel

Kuhusu safari ya ujumbe wa Bahrain ulioitembelea Israel hivi karibuni, Sayyid Hassan Nasrullah amesema viongozi wa utawala wa Aal-Khalifa waliofanya safari hiyo ilikuwa ni kwa malengo yao ya kibanfsi na wala sio kwa niaba ya Wabahrain na wanazuoni wa nchi hiyo.

Kwengineko katika hotuba yake hiyo amesema moja ya radiamali zenye izza kwa kitendo hicho cha Trump ni kuutenga kwa kila namna utawala wa Kizayuni wa Israel.