Dec 13, 2017 03:55 UTC
  • UNICEF yataka watoto wanaotumia intaneti walindwe

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF linasema wakati fursa ya matumizi ya mtandao wa intaneti ikiongezeka ni lazima dunia hii ya kidijitali iyafanye matumizi hayo kuwa salama kwa watoto ili yaweze kunufaisha hasa wale walio katika hatari zaidi.

Ripoti mpya ya UNICEF iliyotolewa wiki hii, inachunguza ustawi wa kidijitali na athari za mtandao na vyombo vya habari vya kijamii kwa usalama na ustawi wa watoto.

UNICEF inasema licha ya uwepo mkubwa wa watoto mtandaoni huku mtumiaji 1 kati ya 3 wa intaneti duniani kote akiwa ni mtoto, ni hatua kidogo sana zilizochukuliwa kuwalinda watoto kutokana na hatari zake na kuongeza fursa yao ya kupata maudhui salama ya mtandao.

Ripoti hiyo iitwayo "Hali ya watoto duniani 2017:watoto katika ulimwengu wa kidijitali" inatoa mtazamo wa kwanza kabisa wa UNICEF katika kuangalia njia tofauti za teknolojia ya kidijitali inavyoathiri watoto, fursa zao za maisha, kubaini hatari na pia fursa.

Ripoti inasema serikali na sekta binafsi hazizingatii kasi ya mabadiliko, hivyo zinawaweka watoto katika hatari mpya na kuwaharibu huku zikiwaacha nyuma mamilioni ya watoto wasiojiweza.

Watoto wa shule nchini Kenya wakiwa na tableti zilizosambazwa shuleni kupitia mradi maalumu wa serikali

Anthony Lake mkurugenzi mkuu wa UNICEF amesema "kwa uzuri na ubaya, teknolojia ya kidijitali sasa ni ukweli usiopingika wa maisha yetu,ulio na changamoto kuu mbili,jinsi gani ya kupunguza madhara na wakati huohuo kuongeza faida za mtandao kwa kila mtoto.”

Hata hivyo ripoti inaonyesha mamilioni ya watoto wanakosa fursa hiyo ya mtandao, takribani theluthi ya vijana milioni 346 duniani hawako mtandaoni na Afrika ikishika mkia kwa vijana 3 kati ya 5 ukilinganisha na 1 kati ya 25 barani Ulaya, hali inayoongeza kutokuwepo usawa na kupunguza uwezo wa watoto kushiriki katika uchumi wa kidijitali.

 

Tags