Mjumbe wa UN: Wanawake Waislamu wa Myanmar wanabakwa hadi kufa
Mwakilishi wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuhusu ukatili wa kingono unaofanywa na jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya na kutoa wito wa kutolewa azimio la Baraza la Usalama la kusitishwa ukatili huo mara moja.
Peramila Patin anayeshughulikia ukatili wa kingono katika maeneo ya vita amesema kuwa, mwanamke mmoja Muislamu wa jamii ya Rohingya amemwambia kuwa, alishikiliwa mateka na jeshi la Myanmar kwa muda wa siku 45 na kubakwa kwa zamu.
Peramila Patin ameongeza kuwa, mwanamke mwingine wa Rohingya amepigwa na kunyanyaswa wakati alipokuwa akibakwa na hatimaye akapoteza uwezo wake wa kuona.
Mjumbe huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa amesema watu walioshuhudia wamesema, wanawake na wasichana wa Kiislamu wamekuwa wakifungwa kwenye miamba au miti na kubakwa na kunajisiwa na wanajeshi wa Myanmar hadi kufa.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, watoto wadogo wanaobakwa na kunajisiwa na jeshi la Myanmar wamekuwa wakitupwa motoni baada ya kufanyiwa uhalifu huo.
Peramila Patin amesema kuna udharura kwa ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutembelea Myanmar na eneo la Koks huko Bangladesh lenye wakimbizi zaidi ya laki sita na 26 elfu wa Kiislamu wa kabila la Rohingya.