Dunia yaafiki pendekezo la Iran la kupambana na misimamo mikali
Azimio lililopendekezwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu 'Dunia Dhidi ya Machafuko na Misimamo Mikali' liliidhinishwa kwa mara ya tatu na kwa kauli moja na nchi zote za dunia Jumatano katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mnamo mwaka 2013 aliposhiriki kwa mara ya kwanza katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kama rais wa Iran, kwa kuzingatia kuenea machafuko na misimamo mikali katika maeneo mbali mbali ya dunia, alipendekeza muungano wa 'Dunia dhidi ya Machafuko na Misimamo Mikali' (WAVE).
Pendekezo hilo liliungwa mkono na nchi mbali mbali duniani na wakati huo liliidhinishwa na nchi 190 duniani. Baada ya pendekezo la Rais wa Iran kubadilishwa na kuwa azimio, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema kila miaka miwili kuwe kunatolewa ripoti kuhusu machafuko na misimamo mikali katika Baraza Kuu.
Kuidhinishwa kwa mara nyingine azimio hilo la dunia dhidi ya machafuko na misimamo mikali ni jambo linaloashiria kuwa nchi za dunia zinazingatia kwa kina tatizo hilo ambalo rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alilidiriki miaka minne iliyopita na kutaka kuwepo muungano wa dunia kwa ajili ya kukabiliana nalo.
Leo sawa na mwaka 2013 wakati Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alipohutubu katika Baraza Kuu na kuwajulisha walimwengu kuhusu misimamo mikali bado kuna udharura na umuhimu wa kuendelezwa ushirikiano wa kukabiliana na tatizo hilo.
Ingawa kwa kuangamizwa kundi hatari la kigaidi la ISIS au Daesh nchini Iraq na Syria kulichukuliwa hatua chanya katika vita dhidi ya misimamo mikali lakini bado kuna umuhimu wa kukabiliana na misimamo mikali na ugaidi hasa kung'oa mizizi ya kifikra ya ugaidi.
Kile kilicho na umuhimu mkubwa hapa ni jitihada za pamoja za kukabiliana na misimamo mikali na ugaidi na pia kujiepusha na chuki na kunasibisha dini au taifa fulani na ugaidi.
Leo kila dini na taifa limedhuriwa na misimamo mikali na ugaidi wa makundi kama ISIS na hivyo kutuhumu dini au taifa fulani kuwa linaunga mkono ugaidi ni jambo lisiloweza kuwa na mchango wowote katika kukabiliana na tatizo hilo.
Misimamo mikali na ugaidi ni tatizo la dunia na pia linatokana na sera za baadhi ya serikali. Kutizama ugaidi kama chombo cha kufikia malengo fulani ni jambo linalopelekea kuenea machafuko na kutuhumu dini, taifa au nchi fulani kuwa inaunga mkono ugaidi ni kujaribu kukwepa ukweli wa mambo.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, misimamo mikali ni tatizo la dunia na hivyo kuna haja ya dunia kuungana dhidi ya machafuko na misimamo mikali ya kufurutu ada. Kwa hivyo kupitishwa tena azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu kukabiliana na tatizo la misimamo mikali na machafuko ni jambo linaloonyesha namna Iran inavyotumia mantiki na ilivyo na uono wa mbali na muhimu zaidi ni kutotuhumiwa dini au taifa lolote kuwa linaunga mkono ugaidi.
Ni katika fremu hiyo ndio Gholamali Khoshroo mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa siku ya Jumatano akaashiria kuidhinishwa tena pendekezo hilo la WAVE katika Baraza Kuu na kusema: "Azimio hilo ni mfano mwingine wa mafanikio ya Iran katika Umoja wa Mataifa."
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa na nafasi muhimu katika vita dhidi ya ugaidi. Kuangamizwa ISIS nchini Syria na Iraq sambamba na dunia kuidhinisha azimio la 'Dunia Dhidi ya Machafuko na Misimamo Mikali' ni nukta inayoashiria mafanikio ya Iran kivitendo na kisiasa. Jitihada za kieneo na kimataifa za Iran zinaashiria kuwa walimwengu wanaitambua Jamhuri ya Kiislamu kama nchi inayotetea amani na usalama duniani.