Israel na Marekani zaafiki mapatano ya 'kuikabili' Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i38247-israel_na_marekani_zaafiki_mapatano_ya_'kuikabili'_iran
Imebainika kuwa, maafisa wa ngazi za juu wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel walifanya mkutano wa siri mjini Washington hivi karibuni, kujadili mikakati eti ya kuikabili na kuidhibiti Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 29, 2017 04:27 UTC
  • Israel na Marekani zaafiki mapatano ya 'kuikabili' Iran

Imebainika kuwa, maafisa wa ngazi za juu wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel walifanya mkutano wa siri mjini Washington hivi karibuni, kujadili mikakati eti ya kuikabili na kuidhibiti Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Vyombo vya habari vya Israel vimetangaza habari ya mkutano huo wa faragha na kufichua kuwa, walioongoza kikao hicho kilichofanyika katika Ikulu ya White House Disemba 12 ni H.R. McMaster, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani na mwenzake wa Israel, Meir Ben-Shabbat.

Inaarifiwa kuwa, pande mbili hizo zilikubaliana kuunda timu za pamoja za kupambana na ushawishi wa Iran katika eneo hili la Mashariki ya Kati.

Duru za karibu na kikao hicho cha kificho zimefichua kuwa, pande mbili hizo zilisaini hati yenye mikakati kadhaa itakayotumika, kuzima kile Tel Aviv inakitaja kuwa 'tishio la Iran'.

Marekani na Israel zimekuwa zikila njama ya kuishambulia kijeshi Iran

Habari zinasema kuwa, timu ya kwanza imepewa jukumu la kuzima eti ushawishi wa Iran nchini Syria, sambamba na kuzuia misaada ya Tehran kwa harakati ya muqawama ya Hizbullah ya Lebanon.

Timu ya pili imetwikwa kazi ya kutumia njia za kidiplomasia na intelijensia kusambaratisha mradi wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani, huku timu ya tatu ikipewa jukumu la kuzima mradi wa makombora ya balestiki ya taifa hili.

Ifahamike kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Hizbullah kufuatia ombi la serikali halali ya Rais Bashar al-Assad zimekuwa zikiliunga mkono jeshi la Syria kukabiliana na magenge ya kigaidi yanayoungwa mkono na Marekani na waitifaki wake tangu mwaka 2011.