Rex W. Tillerson: Korea Kaskazini inamkosesha usingizi Trump
https://parstoday.ir/sw/news/world-i38261-rex_w._tillerson_korea_kaskazini_inamkosesha_usingizi_trump
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex W. Tillerson amesema kuwa, Korea Kaskazini ndio tishio kubwa kwa usalama wa Marekani na kwamba, tangu Rais Donald Trump wa Marekani alipoingia madarakani amekuwa akiwaza sana juu ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 29, 2017 12:20 UTC
  • Rex W. Tillerson: Korea Kaskazini inamkosesha usingizi Trump

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex W. Tillerson amesema kuwa, Korea Kaskazini ndio tishio kubwa kwa usalama wa Marekani na kwamba, tangu Rais Donald Trump wa Marekani alipoingia madarakani amekuwa akiwaza sana juu ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Tillerson, tangu Trump alipoingia madarakani amekuwa akiitaja sana serikali ya Pyongyang kuwa ni tishio kuu kwa usalama wa Marekani. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amedai kwamba, tangu Trump alipoachana na siasa za 'subira ya kistratijia' dhidi ya Korea Kaskazini na badala yake kufuata siasa za 'mashinikizo kupitia vikwazo vya kiuchumi' Pyongyang inahisi kwamba inasukumwa kwenda kwenye meza ya mazungumzo ya kweli kwa ajili ya kuachana na miradi ya silaha za nyuklia na makombora yake ya balestiki.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kulia

Hata hivyo serikali ya Korea Kaskazini kwa mara kadhaa imekuwa ikisisitiza kwamba, maadamu Washington na washirika wake hawaachani na vitisho vyao dhidi ya nchi hiyo, Pyongyang itaendelea kujiimarisha kijeshi na uwezo wake wa kimashambulizi. Kadhalika Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amezungumzia uhusiano wa Russia na kudai kwamba Moscow imekuwa ikiingilia masuala ya nchi jirani kama Georgia na Ukraine. Amedai kuwa, katika anga kama hiyo mahusiano ya Marekani na Russia hayawezi kuwa mazuri.

Rais Donald Trump wa Marekani

Hatua ya eneo la Crimea kujitenga na Ukraine na kujiunga na ardhi ya Russia iliyofanyika mwaka 2014 kupitia kura ya maoni iliyoungwa mkono na Moscow, ndio chanzo cha kushtadi mgogoro kati ya Marekani na Russia hadi leo.