Wamarekani wapanga foleni ndefu kununua kitabu kinachomshambulia Trump
Shirika la habari la Associated Press la nchini Marekani limetangaza habari inayosema kuwa wananchi wengi wa nchi hiyo wamepanga foleni ndefu wakisubiri kwa hamu kununua kitabu kinachomshambulia rais wa nchi hiyo, Donald Trump.
Shirika hilo limeripoti kutoka Washington DC kwamba wananchi wamepanga foleni katika maduka ya vitabu wakisubiri kwa hamu kubwa kununua kitabu kinachoitwa “Fire and Fury" cha Michael Wolfe ambacho kinazungumzia mwaka wa kwanza wa urais wa Trump katika Ikulu ya nchi hiyo White House.

Shirika lililochapisha kitabu hicho linasema kuwa, wananchi wengi sana wameonesha hamu ya kununua kitabu hicho hivyo limelazimika kusogeza mbele tarehe ya kuchapishwa kwake kutoka tarehe Mosi hadi tarehe Tano Januari huko Washington.
Kitabu hicho kinachora picha inayoonesha udhalili wa rais wa Marekani Donald Trump na ukosefu wake mkubwa wa heshima alioudhihirisha zaidi baada ya kuingia katika Ikulu ya nchi hiyo. Kitabu hicho kinamuonesha Trump kuwa mtu mwenye fikra za kitoto ambaye hakutarajia kabisa kushinda urais na kuingia katika Ikulu ya White House.
Kitabu hicho kimevutia Wamarekani wengi ambao wamepanga foleni kwenye maduka ya vitabu wakisubiri kwa hamu kukinunua.