Rais Santos wa Colombia: Trump huwezi kuongoza nchi kwa Twitter
Rais Juan Manuel Santos wa Colombia amesema kuwa, siasa na mahusiano ya kigeni hayawezi kuongozwa kwa mtandao wa kijamii wa Twitter.
Rais Santos ameyasema hayo mjini Davos, Uswisi ambapo alikuwa akizingumzia mwenendo wa Rais Donald Trump wa Marekani wa kutumia mtandao huo wa kijamii katika mahusiano ya kigeni ya nchi yake na mataifa mengine ya dunia na kusema, siasa na mahusiano ya kigeni hayawezi kuongozwa kwa njia hiyo, kwani Twitter ni dhihirisho la hisia na kwa msingi huo mtandao huo hauendani na udiplomasia.
Kadhalika Rais Manuel Santos wa Colombia amesema ikiwa Marekani itataka kujitenga yenyewe na bila kuamiliana na nchi nyingine, basi ni Washington ambayo itapata madhara zaidi. Aidha amesisitiza kwamba, ikiwa serikali itataka kutetea maslahi ya nchi yake ni lazima iwe na harakati chanya katika ngazi ya kimataifa, na kwa msingi huo ushirikiano mzuri wa Washington na dunia, utakuwa ni kwa maslahi kwa Marekani pia. Kadhalika Rais Santos ameashiria mustakbali wa mkataba wa NAFTA, ambao ni mkataba wa biashara huria kati ya Amerika ya Kaskazini yaani Mexico, Marekani na Canada na kusisitiza kuwa hatua ya Trump ya kuiondoa nchi yake katika mkataba huo, haitakuwa na maslahi kwa upande wowote.