"Trump ni hatari kwa dunia, yumkini asimalize muhula wake"
Mwekezaji bilionea mashuhuri wa Marekani, George Soros ameutaja utawala wa Rais Donald Trump kama hatari kwa dunia, na kusisitiza kuwa, kushtadi upinzani dhidi ya kiongozi huyo kutamfanya asahaulike kabisa duniani kufikia mwaka 2020 au hata kabla ya hapo.
Kwa mujibu wa televisheni ya CNBC, Soros mwenye umri wa miaka 87 ameushambulia vikali utawala wa Trump, alipokuwa akihutubu katika Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi unaofanyika mjini Davos nchini Uswisi.
Ameonya kuwa, yumkini Marekani ikajitumbukiza katika vita vya nyuklia, kutokana na namna Trump anavyoichangamkia kadhia ya nyuklia ya Korea Kaskazini, huku akikataa kwa makusudi kukubali kuwa Pyongyang ni mmiliki mpya wa silaha za nyuklia.
Bilionea huyo raia wa Marekani mwenye asili ya Hungary amebainisha kuwa, mfumo wa uongozi wa Trump sio hatari tu kwa Wamarekani, bali kwa mfumo mzima wa ustaarabu kote duniani.
Kadhalika ametahadharisha kuwa, iwapo Trump ataendelea na mtindo wake huo wa uongozi, kuna uwezekano mkubwa asiweze kumaliza hata muhula wake wa kwanza.