Wasiwasi wa UN kuhusu kurejeshwa kwa nguvu wakimbizi Waislamu wa Rohingya
Umoja wa Mataifa umesema una wasiwasi mkubwa na suala la kufukuzwa kutoka Bangladesh wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya wa Myanmar.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa imeeleza kwamba, umoja huo una wasiwasi mkubwa na taarifa za kurejeshwa kwa nguvu wakimbizi Waislamu wa Myanmar.
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limetangaza kuwa, kufukuzwa kutoka Bangladesha wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya na kurejeshwa kwa nguvu nchini Myanmar ni jambo linalotia wasiwasi mkubwa mno.
Taarifa ya UNHCR imeeleza kuwa, kuna haja ya kudhaminiwa usalama na kuandaliwa mazingira ya kurejea nchini Myanmar wakimbizi hao Waislamu wa jamii ya Rohingya na sio kulazimishwa kurejea wakati usalama wao haujadhaminiwa.
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR linasema kwamba, hali katika mkoa wa Rakhine nchini Myanmar si shwari kuweza kuwapokea malaki ya wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya waliokimbilia nchini Bangladesh.
Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi hiyo tarehe 25 Agosti mwaka jana hadi sasa.
Hivi karibuni serikali ya Bangladesh ilitangaza kuwa, wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya waliopata hifadhi nchini humo kufuatia ukatili wanaotendewa nchini Myanmar, sasa wamefika milioni moja na idadi hiyo ni kubwa zaidi ya ile ambayo imekuwa ikitajwa katika vyombo vya habari.