Russia yaponda madai ya Marekani dhidi ya Syria
(last modified Sun, 04 Feb 2018 02:43:00 GMT )
Feb 04, 2018 02:43 UTC
  • Russia yaponda madai ya Marekani dhidi ya Syria

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imekadhibisha madai ya Marekani kwamba Syria imetengeneza na kutumia kizazi kipya cha silaha za kemikali na kusema madai hayo hayana msingi wowote.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesema tuhuma hizo za Marekani zinalenga kumchafua Rais Bashar Assad wa Syria.

Taarifa hiyo imesema Washington inatumia tuhuma hizo ili kutenga bomu la ardhini katika mchakato wa mazungumzo ya kisiasa ya kurejesha amani na mapatano nchini Syria.

Taarifa hiyo ya Russia imetolewa baada ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani, James Mattis kuwaambia waandishi wa habari kwamba nchi yake ina wasiwasi kuhusu matumizi ya gesi ya sarin nchini Syria na kwamba wizara yake inachunguza suala hilo. Hata hivyo amekiri kuwa Marekani haina ushahidi wowote wa kuthibitisha madai hayo.

James Mattis

Waziri wa Ulinzi wa Marekani ameashiria kwamba nchi yake yumkini ikafanya mashambulizi dhidi ya Syria iwapo itathibitika kuwa serikali ya nchi hiyo imetumia gesi ya sarin.  

Aprili mwaka jana Marekani ilishambulia uwanja wa ndege wa Jeshi la Anga la Syria wa Shayrat huko Homs kwa makombora 59 aina ya Tomahawk kwa madai kwamba serikali ya Damascus imefanya mashambulizi ya silaha za kemikali kaskazini mwa nchi hiyo. Syria ilikanusha vikali madai hayo.