Jeshi la Myanmar: Waislamu Warohingya watakuwa salama katika maeneo waliyoainishiwa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i44102-jeshi_la_myanmar_waislamu_warohingya_watakuwa_salama_katika_maeneo_waliyoainishiwa
Mkuu wa majeshi ya Myamnar amedai kuwa, wakimbizi Waislamu Warohingya wanaorejea nchini humo watakuwa salama madhali tu watabakia katika kambi na vijiji walivyoainishiwa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 06, 2018 02:35 UTC
  • Jeshi la Myanmar: Waislamu Warohingya watakuwa salama katika maeneo waliyoainishiwa

Mkuu wa majeshi ya Myamnar amedai kuwa, wakimbizi Waislamu Warohingya wanaorejea nchini humo watakuwa salama madhali tu watabakia katika kambi na vijiji walivyoainishiwa.

Jenerali Min Aung Hlaing amedai alipokutana na  ujumbe wa Umoja wa Mataifa kwamba: Hakuna haja ya kuhofia usalama wa wakimbizi hao Waislamu watakaporejea nchini kwao endapo watabakia katika maeneo hayo waliyoainishiwa.

Afisa huyo wa ngazi za juu katika jeshi la Myanmar ambaye anadhibiti masuala yote ya usalama wa nchi hiyo amewapachika Waislamu wa Rohingya jina la "wahamiaji haramu kutoka Bangladesh au Wabangali" licha ya vizazi na vizazi vya jamii hiyo kuishi kwa miaka mingi katika nchi hiyo.

Aidha Mkuu wa Majeshi ya Myanmar amepinga kile alichokiita "utiaji chumvi" ripoti za idadi ya Waislamu Warohingya waliobakwa, kunajisiwa au kuuawa na vikosi vya serikali, licha ya kuweko ushahidi wa wazi wa kuthibitisha hilo.

Waislamu Warohingya wakiyakimbia makazi yao kukwepa hujuma za jeshi na mabudha dhidi yao

Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa  ambao hivi karibuni ulifanya safari nchini Bangladesh na Myanmar, umetoa wito wa kufanyika "uchunguzi unaostahiki" kuhusiana na madai ya kufanyika jinai dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa nchi hiyo.

Serikali ya Myanmar imekuwa ikiandamwa na ukosoaji mkali tangu jeshi lake na magenge ya Mabudha walipoanzisha hujuma na mashambulio dhidi ya Waislamu Warohingya ambao ni jamii ya waliowachache nchini humo. Maelfu ya Waislamu Warohingya wameuawa hadi sasa na wengine wapatao laki saba wamekimbilia katika nchi jirani ya Bangladesh tangu Agosti mwaka jana.