Rais Frank-Walter Steinmeier: Ujerumani tunaunga mkono makubaliano ya JCPOA
Rais Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani amesisitiza kuwa, nchi yakke inaunga mkono makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na Iran na pia udharura wa kubakishwa makubaliano hayo.
Rais Frank-Walter Steinmeier ameashiria mivutano ya Rais Donald Trump wa Marekani na Umoja wa Ulaya kuhusiana na makubaliano ya nyuklia na Iran na kueleza wasiwasi wake juu ya kutokea mabadiliko makubwa katika uhusiano wa pande mbili hizo.
Rais wa Ujerumani amesema bayana kwamba, endapo makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yatavurugika na kisha kujitokeza mashindano mapya ya kumiliki silaha katika Mashariki ya Kati, eneo hili halitaweza tena kustahamilimachafuko mengine.
Rais Frank-Walter Steinmeier ameongeza kuwa, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa walichukua hatua sahihi huko Washington kwani suala la maslahi ya Ulaya lilizingatiwa na wakati huo huo wakasisitiza udharura wa kulindwa na kutekelezwa makubaliano ya nyuklia na Iran.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Rais Hassan Rouhani jana alisisitiza kuwa, makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ambao ni mkataba wa kimataifa na dhihirisho la nguvu za kidiplomasia za taifa kubwa la Iran hauwezi kufanyiwa mabadiliko yoyote.
Makubaliano ya nyuklia, yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) yaliyofikiwa kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi sita zinazounda kundi la 5+1, ambazo ni Uingereza, Ufaransa, Russia, China, Marekani na Ujerumani, yalianza kutekelezwa Januari 2016, lakni serikali ya Marekani imekuwa ikihalifu kuyatekeleza. Aidha rais wa nchi hiyo Donald Trump anataka makubaliano ya JCPOA yafanyiwe mabadiliko, la sivyo Marekani itajitoa kwenye makubaliano hayo.