Ubeberu mpya wa Marekani na majibu makali ya Japan
Ubeberu mpya wa Marekani uliozikasirisha nchi waitifaki na wapinzani wake zikiwemo za Ulaya pamoja na China na Russia, umekuwa mkubwa kiasi kwamba hata Japan na Korea Kusini ambazo ni waitifaki wakubwa wa Washington nao wameshindwa kunyamaza na wametishia kuchukua hatua kali kujibu kuongezewa ushuru bidhaa zao zinazoingia nchini Marekani.
Baada ya Marekani kutangaza ushuru mpya kwa bidhaa za Japan zinazoingia nchini humo tena kinyume kabisa na miamala ya kibiashara ya kimataifa, Tokyo nayo imesema itachukua hatua kama hizo kujibu ubeberu huo mpya wa Marekani. Msemaji mkuu wa serikali ya Japan, Yoshihide Suga alisema juzi Alkhamisi kuwa, majibu ya Tokyo kwa ubeberu huo mpya wa Marekani yatakuwa mazito hasa kwa kuzingatia kuwa hata Korea Kusini ambayo nayo ni muitifaki wa Marekani imeazimia kuchukua hatua kama hizo kujibu ushuru mpya uliotangazwa na Marekani kwa bidhaa zake.
Yoshihide Suga amesema kuwa, Japan itachukua hatua zozote zinazohitajika chini ya msingi wa sheria za Shirika la Kimataifa la Biashara kwa ajili ya kulinda manufaa yake ya kibiashara mbele ya ubeberu mpya wa Marekani.
Amesema: Kwa muda mrefu sasa Japan imekuwa ikiinasihi Marekani isichukue hatua hizo lakini Washington inaendelea kuwa mkaidi hivyo Tokyo imeamua kuchukua hatua kama hizo kukabiliana na ushuru huo mpya wa Marekani. Nchi zote zilizokumbwa na panga hilo jipya la Marekani zimeamua kuchukua hatua kama hizo kujibu ubeberu na siasa za rais wa Marekani Donald Trump za kujikumbizia kila kitu upande wake.
Kama tulivyoashiria huko nyuma, hatua za kupambana na ubeberu mpya wa Marekani zimechukuliwa na hata nchi marafiki wa karibu wa nchi hiyo kama Japan na Korea Kusini.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa siasa za kibeberu za Marekai hazijali rafiki wala adui kwani kwa nchi kama Japan ambayo imewekewa masharti ya kuilipa Marekani gharama za kuungwa mkono na licha ya kwamba Tokyo ni miongoni mwa wanunuzi wa daima wa huduma za usalama za Washington, lakini pamoja na hayo haikusalimika na jambia la ushuru mkubwa uliowekwa na Marekani kwa bidhaa zzinazoingia nchini humo. Ikumbukwe pia kuwa, hatua hiyo ya Washington inakinzana waziwazi na sheria za biashara ya kimataifa na biashara huru ambayo Marekani imekuwa ikiisisitizia sana.
Siasa mpya za Marekani za kuhodhi kila kitu hasa katika masuala ya biashara na uchumi zimelalamikiwa na hata mashirika ya ndani ya Marekani kwenyewe ambayo yamehisi hatari ya kupoteza manufaa yao kimataifa. Katika siasa zake mpya, Trump amezingatia tu ni kiasi gani Marekani itaingiza faida bila ya kujali hasara ambazo zitabebwa na marafiki zake, au hata madhara ya muda mrefu ambayo mashirika ya ndani ya Marekani yatapata ikiwa ni pamoja na kupoteza wateja wake. Itakumbukwa kuwa hata Umoja wa Ulaya kupitia kikao chake cha hivi karibuni cha viongozi wakuu wa nchi wanachama umesema kuwa utasimama kidete kukabiliana na ubeberu huo mpya wa Marekani. Wachambuzi wa mambo aidha wanasema, iwapo nchi zote zilizoongezewa ushuru na Marekani zitajibu sawa na hatua hizo za Washington, basi upande wa kwanza utakaopata hasara kubwa zaidi na Marekani yenyewe.
Mtaalamu wa uchumi, David McWilliams anasema: Siasa mpya za ushuru za Trump ambazo bila ya shaka zitakumbwa na majibu makali ya washirika wake wa kibiashara, zitakuwa na madhara makubwa kwa uchumi wa Marekani.
Msimamo wa Japan wa kutoa majibu makali kwa ubeberu mpya wa Marekani unaonesha kuwa, licha ya kwamba Tokyo ni rafiki mkubwa wa Washington, lakini haiko tayari kumezwa na ubeberu wa nchi hiyo na imejiwekea mistari myekundu ya kulinda maslahi na haki yake ya kujitawala kama ambavyo siasa hizo mpya za Marekani zinazidi kuwathibitishia walimwengu kuwa Marekani si dola linaloweza kuaminiwa hata kidogo.