Uamuzi wa Umoja wa Ulaya wa kuwawekea vikwazo viongozi wa Myanmar
Hatimaye mateso na masaibu wanaykabiliana nayo Waislamu wa kabila la Rohingya wa nchini Myanmar yameupelekea Umoja wa Ulaya kutekeleza vikwazo kwa viongozi wa Myanmar.
Umoja wa Ulaya leo umetangaza kuwa Brussels ina mpango wa kuwawekea vikwazo viongozi wa Myanmar kwa kuzingatia hali inayowakabili Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar. Kwa msingi huo, Umoja wa Ulaya unatazamia kuwaweka katika orodha yake ya vikwazo viongozi saba wa kijeshi wa Myanmar. Kwa mujibu wa vikwazo hivyo ni kuwa, fedha za maafisa hao zitazuiwa na hawataruhusiwa kufanya safari katika nchi za Ulaya.
Jeshi la Myanmar huku likishirikiana na Mabudha wenye misimamo mikali wa nchi hiyo wanatuhumiwa kutekeleza hujuma za ukandamizaji na utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu wa Rohingya sambamba na kuwabaka watoto na wanawake wa kabila hilo la Rohingya.
Takwimu zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Population Fund zinaonyesha kuwa zaidi ya wanawake Waislamu wa kabila la Rohingya elfu 13 wamekabiliwa na hujuma za mateso na kubakwa baada ya kuyakimbia makazi yao wakati wakitafuta hifadhi. Aidha Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef) limebainisha kuwa kwa siku akina mama huzaa karibu vichanga 60 katika kambi za wakimbizi. Watoto hao huzaliwa na akina mama ambao walibakwa wakati wakitafuta hifadhi.