Wasiwasi wa kukiukwa haki za binadamu nchini Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i46480-wasiwasi_wa_kukiukwa_haki_za_binadamu_nchini_marekani
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limekosoa siasa za hivi karibuni za serikali ya Marekani kuhusiana na haki za binadamu na kusisitiza kuwa serikali ya Washington imeliweka kando suala la haki za binadamu katika uga wa siasa za ndani na nje.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jun 30, 2018 12:35 UTC
  • Wasiwasi wa kukiukwa haki za binadamu nchini Marekani

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limekosoa siasa za hivi karibuni za serikali ya Marekani kuhusiana na haki za binadamu na kusisitiza kuwa serikali ya Washington imeliweka kando suala la haki za binadamu katika uga wa siasa za ndani na nje.

Japokuwa suala la kutoheshimu haki za binadamu na sheria za kimataifa ni jambo lenye historia katika rekodi ya utendaji ya Marekani, lakini baada ya kuingia madarakani Rais Donald Trump mwezi Januari mwaka jana na kuchukua maamuzi  ya kuwapiga marufuku raia wa baadhi ya nchi za Kiislamu kufanya safari nchini Marekani, kutekeleza siasa kali dhidi ya wahajiri, kuwatenganisha kwa lazima watoto na wazazi wao wasio na vibali halali vya uhajiri na hatimaye kujitoa katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa; yote hayo yamedhihirisha kwa uwazi zaidi namna viongozi wa Marekani wanavyopuuza suala la haki za binadamu.  

Watoto wahajiri waliotenganishwa na wazazi wao nchini Marekani 

Sarah Margon ambaye ni mwakilishi wa shirika la Human Rights Watch mjini Washington anaeleza kuwa: Katika zama hizi za utawala wa Rais Trump tunashuhudia mabadiliko na matukio makubwa ya jinsi Marekani inavyoamiliana na suala la haki za binadamu ndani ya nje ya nchi hiyo, kiasi kwamba hakuna Rais  yeyote wa Marekani ambao aliwahi kufikia kiwango kama hiki cha kudharau haki za binadamu na kutoa matamshi ya fedheha kuhusu masuala ya haki hizo. 

Sarah Margon, Mwakilishi wa Shirika la Human Rights Watch mjini Washington 

Tukitazama kwa ujumla mazingira ya sasa tunaweza kubaini ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaojiri ndani na nje ya Marekani. Ndani ya Marekani kwenyewe, kuendelea vitendo vya kibaguzi vinavyofanywa na viongozi wa nchi hiyo dhidi ya raia wasio wazungu, mienendo yao mibaya dhidi ya wahajiri hususan uamuzi wa hivi sasa wa Rais wa Marekani wa kuwatenganisha watoto wahajiri na wazazi wao na kisha kuwaweka katika kambi zisizofaa, kuwapiga marufuku raia wa nchi sita wa Kiislamu kufanya safari nchini Marekani, kukabiliana na baadhi ya vyombo vya habari na kuzitaja habari za vyombo hivyo kuwa za uwongo; yote hii ni mifanyo ya wazi kabisa ya ukiukaji wa haki za binadamu na uhuru nchini humo. Aidha kupuuza haki za wafungwa na kuweka vizuzi vya kuwanyima wafungwa hao haki zao za kisheria ni ukiukaji mwingine wa haki za binadamu unaoshuhudiwa huko Marekani. 

Stephen Landman mchambuzi na mwanahistoria mtajika wa Marekani anasema kuhusu rekodi ya haki za binadamu ya Marekani kwamba: "Hakuna nchi katika historia ya dunia iliyowasababisha maafa makubwa watu kama Marekani. Demokrasia ya Marekani ni njozi tupu inayobeba jina la demokrasia", mwisho wa kunukuu  

Wakati huo huo katika uga wa nje pia Marekani imekuwa ikifuatilia malengo yake maovu bila ya kuzingatia thamani, sheria na haki za kimataifa na ili kutimiza malengo yake hayo, nchi hiyo imekuwa ikikiuka pakubwa na waziwazi haki za binadamu katika nchi nyingine. Mfano wa karibuni kabisa wa kadhia hii ni kujiondoa nchi hiyo katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa. Marekani ni nchi ya kwanza iliyojitoa katika baraza hilo la haki za binadamu. Wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, kujitoa Marekani katika baraza hilo ni ishara ya kujiweka mbali viongozi wa Washington na suala la kuheshimu haki za binadamu. Uungaji mkono wa Marekani kwa Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni wa Israel na siasa zilizo dhidi ya binadamu ya nchi hizo, ni kadhia nyingine inayodhihirisha namna Marekani inavyokiuka pakubwa haki za binadamu duniani. 

Ripoti ya karibuni ya shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch imethibitisha ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na Marekani. Hii ni katika hali ambayo viongozi wa Marekani siku zote wamekuwa wakidai kuwa nchi hiyo ni miongoni mwa vinara wa kutetea haki za binadamu duniani.

Katika mazingira hayo, inaonekana kuwa viongozi wa Marekani wanatumia suala la haki za binadamu kama wenzo wa kufikia malengo yao ya kutaka kuingilia masuala ya nchi nyingine na kuzusha mizozo katika nchi hizo.