Msalaba Mwekundu: Myanmar sio salama kurejea wakimbizi wa Rohingya
Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu imesema sio salama kwa maelfu ya wakimbizi wa Rohingya wanaoshi kambini katika nchi jirani ya Bangladesh kurejea makwao katika mkoa wa Rakhine nchini Myanmar.
Peter Maurer, Rais wa shirika hilo aliyasema hayo jana Jumapili na kuongeza kuwa, mengi yanahitajika kufanywa ili kuboresha hali aliyoishuhudia mwenyewe alipofanya ziara rasmi katika mkoa huo hivi karibuni.
Amesema sharti mazingira yaandaliwe kabla ya kuanzisha mchakato wa kuwarejesha kwa hiari Warohingya wanaoishi kati hali ya kutamausha katika kambi za wakimbizi nchini Bangladesh.
Amesema: Yale niliyoyashuhudia kuanzia masoko na vijiji vilivyoharibiwa kikamilifu kwa kuteketezwa kwa moto, majumba gofu, hali ya kijamii na kimazingira, sidhani ni wakati mwafaka wa kurejea kwa wakimbizi wa Rohingya.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ambaye jana Jumapili alifanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Bangaldesh, Sheikh Hasina mjini Dhaka kuhusu hali ya wakimbizi hao wa Kirohingya, anatazamiwa kuzitembelea kambi za wakimbizi hao leo Jumatatu, ikiwa ni mara yake ya kwanza kufanya hivyo.
Bangladesh ina wakimbizi Waislamu zaidi ya laki saba kutoka jamii ya Rohingya nchini Myanmar ambao wamekimbilia katika nchi hiyo jirani kutokana na maudhi, mateso na hata mauaji dhidi yao yanayofanywa na jeshi na Mabudha wenye misimamo ya kuchupa mipaka.
Wakimbizi hao wanakabiliwa na hali mbaya kutokana na kuishi katika mazingira mabovu katika kambi za wakimbizi na kulemewa serikali ya Dhaka kubeba mzigo wa wakimbizi hao.