Sisitizo la Trump la kuzidi kuzibana kiuchumi nchi za Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i47657-sisitizo_la_trump_la_kuzidi_kuzibana_kiuchumi_nchi_za_ulaya
Rais wa Marekani, Donald Trump amesisitizia utekelezaji wa ilani yake ya uchaguzi ya "Marekani Kwanza" na ameahidi kuendelea kuzibana kiuchumi nchi za Ulaya kwa ajili ya kurejesha kile alichodai ni nguvu za Marekani zilizopotea.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 24, 2018 08:54 UTC
  • Sisitizo la Trump la kuzidi kuzibana kiuchumi nchi za Ulaya

Rais wa Marekani, Donald Trump amesisitizia utekelezaji wa ilani yake ya uchaguzi ya "Marekani Kwanza" na ameahidi kuendelea kuzibana kiuchumi nchi za Ulaya kwa ajili ya kurejesha kile alichodai ni nguvu za Marekani zilizopotea.

Utekelezaji wa ilani hiyo ya Donald Trump unawajibisha kuongezewa ushuru bidhaa za kigeni zinazoingia Marekani suala ambalo limezusha vita vikubwa vya kiuchumi ulimwenguni. Hatua ya Marekani ya kuziongezea ushuru wa asilimia 25 na asilimia 10 bidhaa za feleji na alumini imewakasirisha mno washirika wa kiuchumi wa Marekani kiasi kwamba na wao wameamua kuchukua hatua kali dhidi ya Washington kujibu uvunjaji huo wa ahadi wa Marekani. Vita hivyo vya kiuchumi ni vikubwa zaidi sasa hivi baina ya Marekani na China. Nchi za Ulaya ambazo ni waitifaki wakubwa wa Marekani nazo hazikusalimika na ubeberu huo wa Washington. Viongozi wa nchi za bara hilo wanasema kuwa, vita vya kiuchumi vilivyoanzishwa na Trump vina madhara kwa pande zote. Uchumi wa nchi za Ulaya hasa Ujerumani unategemea usafirishaji nje bidhaa, hivyo nchi za bara hilo zimepata hasara kubwa kutokana na siasa mpya za Trump. Hata hivyo baada ya Jean-Claude Juncker, mkuu wa kamisheni ya Ulaya kutembelea Marekani na kuzungumza na Trump, hivi sasa kuna mapatano angalau ya muda yamefikiwa baina ya Ulaya na Washington. Mapatano hayo yamefikiwa baada ya miezi kadhaa ya mizozo baina ya Ulaya na Marekani; mizozo ambayo ilikuwa mikubwa kiasi kwamba Trump alidai kuwa nchi za Ulaya ni maadui wa kiuchumi wa Marekani. Licha ya kufikiwa mapatano hayo ya muda, lakini bado kuna wasiwasi mkubwa kuhusu suala hilo. Katika msimamo wake wa karibuni kabisa ambao unahatarisha mapatano hayo ya muda, Trump amesema kuwa, ana nia ya kuyapandishia ushuru wa asilimia 25 magari ya nchi za Ulaya yanayoingia Marekani.

Rais wa Marekani Donald Trump analaaniwa katika kila kona ya dunia

 

Trump amesema: Tunafuatilia suala la kuiongezea ushuru wa asilimia 25 kila gari inayotoka Umoja wa Ulaya na kuingia Marekani.

Hii si mara ya kwanza kwa Trump kutishia kuongeza ushuru wa bidhaa yakiwemo magari ya nchi za Ulaya yanayoingia Marekani. Kwa mara ya kwanza mwezi Mei 2018, Trump alitishia kuongeza ushuru wa magari hayo na aliitaka wizara ya biashara ya Marekani kutathmini iwapo uingizaji wa magari nchini humo ni tishio kwa usalama wa taifa wa nchi hiyo au la. Hata hivyo ukweli wa mambo ni kama wanavyosema viongozi wa Ulaya kuwa siasa hizo za Trump zina madhara kwa pande zote kwani licha ya kwamba kuongezewa ushuru magari ya Ulaya yanayoingia Marekani kunaweza kuviweka katika wakati mgumu viwanda vya kutengeneza magairi na wafanyakazi wa viwanda hivyo huko Ulaya, lakini katika upande wa pili pia, madhara ya jambo hilo yatawakumba watumiaji wa magari ndani ya Marekani kwenyewe. Si hayo tu, lakini bila ya shaka nchi za Ulaya nazo zitalipiza kisasi cha kuyaongezea ushuru magari ya Marekani yanayoingia katika nchi hizo kwa kiwango kisichopungua hicho hicho kilichoongezwa na Trump. Vile vile, kuna mashirika mengi ya kigeni ya kutengeneza magari huko Marekani likiwemo shirika la BMW la Ujerumani ambalo linahesabiwa kuwa moja ya mashirika makubwa yanayozalisha magadi huko Marekani. BMW imetoa fursa nyingi za kazi kwa wananchi wa Marekani hivyo kupungua uzalishaji wa shirika hilo kuna madhara ya moja kwa moja kwa raia wa Marekani walioajiriwa na BMW. Kwa maneno ya wazi zaidi ni kwamba, kama Trump ataongeza ushuru huo atakuwa amepoteza nafasi laki moja na 90 elfu za kazi ndani ya Marekani kwenyewe. Bei ya magairi ya Ulaya nayo itapanda kutoka dola 1400 hadi dola 7000 kila gari moja. 

Trump akicheza ngoma na viongozi wa Saudia baada ya kukaribishwa kwa heshima zote na ukoo wa Aal Saud licha ya kwamba analaaniwa katika kila kona ya dunia

 

Hata hivyo hadi hivi sasa haijajulikana uamuzi huo wa Trump utaanza kutekelezwa lini. Wilbur Ross, waziri wa biashara wa Marekani amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na Wall Street Journal kwamba, mazungumzo yanaendeelea hivi sasa baina ya Marekani na Umoja wa Ulaya, Mexico na Canada kuhusu kuakhirishwa nyongeza hiyo ya ushuru.

Itakumbukwa kuwa mwaka jana pekee, Marekani iliingiza kutoka nje magari makubwa na madogo yenye thamani ya dola bilioni 200. Asilimia 80 ya magari hayo yalitoka Ujerumani, Mexico, Canada na Japan. Nchi za Ulaya zinaisimanga Marekani kwa kuiambia, si tu mashirika yao ya kuzalishaji magari yameandaa nafasi nzuri za kazi kwa raia wa Marekani, bali pia yametoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya kiteknolojia ya nchi hiyo.