Uturuki: Tutaendelea kushirikiana na Iran licha ya Marekani kuiwekea vikwazo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki amesema kuwa, Ankara haitojali vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran na itaendeleza ushirikiano wake na Tehran kama kawaida.
Mevlüt Çavuşoğlu alisema hayo jana alipohojiwa na shirika la habari la Sputnik mjini New York, Marekani na huku akijibu swali kwamba je, Uturuki itatekeleza vikwazo vya Marekani dhidi ya sekta ya mafuta ya Iran amesema, sisi hatuungi mkono vikwazo na tutaendelea kufanya biashara zetu kama kawaida na Iran.
Çavuşoğlu ameongeza kuwa, Uturuki ni nchi huru yenye haki ya kujiamulia yenyewe mambo yake na iko tayari kushiriki tu katika vikwazo vinavyowekwa na Umoja wa Mataifa na si kinyume na hivyo.
Tarehe 8 Mei mwaka huu, rais wa Marekani, Donald Trump alirudia tuhuma zake zisizo na msingi dhidi ya Iran na kuamua kuitoa Washington katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na hapo hapo akatangaza kurejesha vikwazo vyote vilivyokuwa vimeondolewa dhidi ya Iran.
Awamu ya kwanza ya vikwazo hivyo ilianza kutekelezwa tarehe 7 Agosti na awamu ya pili ambayo inahusu sekta ya mafuta ya Iran itaanza kutekelezwa tarehe 4 Novemba mwaka huu.
Hata hivyo ujuba na ubeberu huo wa Marekani ambao unakanyaga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa umepingwa vikali kote duniani kiasi kwamba nchi mbalimbali zimetangaza kuwa hazitotekeleza vikwazo hivyo vya Marekani dhidi ya Iran.