Marekani, adui wa amani na usalama wa dunia
Uamuzi uliochukuliwa na Rais Donald Trump wa Marekani wa kujiondoa katika mkataba wa silaha za nyuklia za masafa ya kati (INF) ambao umechukuliwa katika fremu ya sera za Trump za kujiondoa katika mikataba ya kimataifa, umekabiliwa na upinzani mkubwa wa viongozi wa nchi na jumuiya mbalimbali za kimataifa.
Kufuatia uamuzi huo, Rais Evo Morales wa Bolivia ameitaja Marekani kuwa ni adui wa amani ya kimataifa na haki za binadamu. Morales ameandika katika ujumbe wake wa Twitter kwamba: Baada ya kutangaza uamuzi wake wa upande mmoja wa kuiondoa Marekani katika mkataba wa INF, Trump ametishia kwamba, atatuma majeshi yake katika mpaka wa nchi hiyo na Mexico ili kuzuia maelfu ya mahajiri wanaotoka America ya Kati kuingia Marekani. Kwa msingi huo Marekani ni adui wa amani ya kimataifa na haki za binadamu.
Rais Evo Morales wa Bolivia ni miongoni mwa wakosoaji wakubwa wa siasa za Marekani na mara kwa mara amekuwa akiituhumu nchi hiyo kuwa inakiuka demokrasia na kuwaunga mkono na kuwahami madikteta. Vilevile amepinga vikali uamuzi wa serikali ya Trump wa kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Japokuwa hadi sasa Trump amechukua hatua za kujiondoa katika makubaliano na mikataba kadhaa ya kimataifa kama mkataba wa hali ya hewa wa Paris, makubaliano ya kimataifa ya kibiashara na mikataba kadhaa ya kisiasa, lakini kuchukua hatua kama hiyo katika mikataba ya kijeshi na usalama wa kimataifa kama uamuzi wake wa kuiondoa Marekani katika mkataba wa silaha za nyuklia za masafa ya kati kunaweza kuzidisha hali ya ukosefu wa amani katika uga wa kimataifa na kuanzisha uwanja wa kuwepo mashindano mapya ya silaha.
Russia ambayo ndiye mshindani mkubwa zaidi wa kijeshi wa Marekani imeutaja uamuzi huo wa Trump kuwa na "hatari sana". Hivi sasa pia bara la Ulaya ambalo katika kipindi cha Vita Baridi lilikuwa medani ya makabiliano na mpambano wa silaha za nyuklia baina ya Marekani na Urusi na lilipata usalama zaidi baada ya kutiwa saini mkataba wa kuondolewa makombora ya nyuklia barani humo, linakabiliwa tena na zimwi na tishio la kupelekwa tena silaha za nyuklia katika eneo hilo.
Marekani ambayo inataka kujiondoa katika mkataba wa INF kwa kutumia madai kuwa Russia imeukiuka na kwa sababu mkataba huo unaizuia Washington kutengeneza silaha mpya za kukabiliana na makombora ya China huko mashariki mwa Asia, sasa haitakuwa na kizuizi chochote katika uwanja huo na itatumia fursa hiyo kupeleka makombora ya nyuklia katika pembe mbalimbali za Ulaya. Hata hivyo inaonekana kuwa, kwa kutilia maanani upinzani wa nchi za Ulaya dhidi ya uamuzi wa Marekani wa kujiondoa katika mkataba wa INF, haitakuwa rahisi kwa serikali ya Washington kuzishawishi nchi za Ulaya zirejee tena katika hali ya kipindi cha Vita Baridi.
Katika uwanja huo na ili kupunguza hatari ya kutokea vita vya silaha za nyuklia barani Ulaya, Kamisheni ya Umoja wa Ulaya imetoa taarifa ikizitaka Marekani na Russia kulinda mkataba wa silaha za nyuklia za masafa ya kati (INF).
Mkataba INF ulitiwa saini mwaka 1987 mjini Washington na kuanza kutekelezwa mwaka 1988. Mkataba huo wa silaha za nyuklia za masafa ya kati unazizuia nchi hizo mbili kuweka makombora ya balestiki na ya Cruise barani Ulaya. Vilevile unasisitiza ulazima wa kuharibiwa makombora ya nyuklia ya masafa ya kati ya kilomita 1000 mpaka 5500 na yale ya masafa mafupi ya kilomita 500 hadi 1000. Vilevile ulizitaka pande hizo mbili kuharibu karibu makombora elfu mbili na 692 hadi kufikia katikati ya mwaka 1991.
Inaonekana kuwa, Marekani imechukua hatua kubwa za kustawisha na kueneza silaha zake za nyuklia si barani Ulaya pekee bali hata katika nchi za mashariki mwa Asia kwa shabaha eti ya kukabiliana na makombora ya China. Suala hili kama, alivyosisitiza Rais Evo Morales wa Bolivia, halitakuwa na matokeo ghairi ya kuhatarisha zaidi amani na usalama wa dunia.