Aghalabu ya Wamarekani wanataka mfumo wa vyama vingi
Akthari ya wananchi wa Marekani wanaona kuwa mfumo wa vyama viwili vya kisiasa una mapungufu na kuna haja ya kuwa na chama au mrengo wa tatu wa kisiasa nchini humo.
Utafiti uliofanywa na kituo cha Gall Up umesema kuwa, asilimia 57 ya Wamarekani wanaona kuwa vyama viwili vya Republican na Democrat havitoshi katika kukiodhi mahitaji ya wananchi na kwamba kuna haja ya kuundwa chama kingine kitakachoangazia maslahi yao.
Asilimia 38 ya watu waliohijiwa kwenye utafiti huo wanasema kuwa, vyama viwili hivyo haviwaridhishi katika utendaji wao na kwa msingi huo, sharti chama cha tatu cha kupigania maslahi yao kibuniwe.
Kwa mujibu wa utafiti huo wa Gall Up, asilimia 72 ya Wamarekani ambao kwa sasa hawaviungi mkono vyama hivyo viwili vya Democrats na Republican wamesema wako tayari kuunga mkono chama au mrengo mpya wa kisiasa.
Mapema mwaka huu, Gavana wa jimbo la Ohio la Marekani, John Kasich alisema katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya ABC ya Marekani kwamba: "Inaonekana hivi sasa tumo katika kufikia mwishoni mwa mfumo wa vyama viwili humu nchini na mimi sitoshangaa nikija kuona mfumo wa vyama vingi unaanza nchini kwetu."
Gavana huyo wa jimbo la Ohio la Marekani aliongeza kuwa, mfumo wa hivi sasa wa vyama viwili hauwezi kutoa majibu ya kuridhisha kwa mahitaji muhimu ya wananchi wa Marekani.