Uchaguzi wa Marekani, matokeo na taathira zake
https://parstoday.ir/sw/news/world-i49349-uchaguzi_wa_marekani_matokeo_na_taathira_zake
Hatimaye baada ya miaka miwili ya Warepublican kuhodhi mihimili yote ya nguvu za madaraka nchini Marekani, moja ya mabaraza mawili yanayounda Kongresi ya nchi hiyo limeingia mikononi mwa chama cha upinzani cha Democrat.
(last modified 2026-08-12T14:02:06+00:00 )
Nov 07, 2018 12:49 UTC
  • Uchaguzi wa Marekani, matokeo na taathira zake

Hatimaye baada ya miaka miwili ya Warepublican kuhodhi mihimili yote ya nguvu za madaraka nchini Marekani, moja ya mabaraza mawili yanayounda Kongresi ya nchi hiyo limeingia mikononi mwa chama cha upinzani cha Democrat.

Kama ilivyokuwa imetabiriwa na aghalabu ya tafiti na chunguzi za maoni, viti vingi vya Baraza la Wawakilishi katika uchaguzi wa katikati ya muhula uliofanyika Novemba 6 vimenyakuliwa na wagombea wa chama cha Democrat, huku Warepublican wakiendelea kulinda wingi wao katika baraza la Seneti.

Zoezi la upigaji kura lilipokuwa likiendelea

Kurejea Wademocrat kwenye nafasi ya waliowengi ndani ya Baraza la Wawakilishi baada ya kupita miaka minane, ikiwa ni baada ya miaka miwili pia tokea Donald Trump awe rais wa Marekani, kutaleta mabadiliko katika sera za ndani na nje, za nchi hiyo. Kushindwa Warepublican katika uchaguzi wa Baraza la Wawakilishi, ambao utambulisho wake ni mpana zaidi kuliko wa Baraza la Seneti, kunaakisi kiwango cha manung'uniko na malalamiko ya Wamarekani kwa serikali ya chama hicho. Na hii ni pamoja na kwamba, Warepublican, na hasa Trump mwenyewe, alikuwa na matumaini kuwa ataweza kuwaridhisha raia wa Marekani na kuvutia uungaji mkono wao kwa kuboresha vielezo vya uchumi na kutekeleza sera kali kuhusiana na uingiaji wa wakimbizi na wahajiri haramu nchini humo. Hata hivyo matokeo ya awali yameonyesha kuwa, karibu asilimia 55 ya wapiga kura katika uchaguzi wa bunge uliofanyika jana Jumanne wamezipigia kura ya 'hapana' siasa na sera za serikali ya Warepublican.

Rais wa Marekani Trump (kushoto) na mtangulizi wake Obama wakiongoza kampeni za wagombea wa vyama vyao

Vyovyote itakavyokuwa, kuanzia Januari 3 mwakani, wakati Kongresi, yaani Bunge la 116 la Marekani litakapoanza shughuli zake, Wademocrat ndio watakaokalia kiti cha Uspika na kuongoza kamati zote za bunge hilo. Na kuanzia hapo hadi miaka miwili itakayofuatia, Trump atakuwa na kibarua kigumu cha kuvuka kizingiti kirefu cha Wademocrat katika Baraza la Wawakilishi, ili kuweza kutekeleza mipango na sera zake. Baraza hilo ndilo takriban linalohodhi uandaaji na upangaji wa bajeti ya serikali kuu ya Marekani, na lina uwezo wa kuiwekea mashinikizo makali Ikulu ya White House katika kufanikisha mipango yake, kwa kutumia turufu ya kubadilisha tarakimu za ukubwa wa bajeti yake. Lakini pia, kulidhibiti Baraza la Wawakilishi, kunawapa Wademocrat fursa ya kipekee, ya kuweza kuchunguza na kufuatilia kashfa kadhaa zinazomkabili Trump, ikiwemo ya tuhuma za kushirikiana kula njama na Russia, kukwepa kulipa kodi na mahusiano yake ya kingono na wanawake kadhaa. Mamlaka hayo watakayokuwa nayo Wademocrat yatawawezesha hata kumtangazia mashtaka rais na kutaka asailiwe na kuuzuliwa na Baraza la Seneti.

Lakini pamoja na hayo, katika tamko la kwanza alilotoa baada ya ushindi wa chama chake, Nancy Pelosi, mbunge wa chama cha Democrat, anayetarajiwa pengine kuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi katika Kongresi ya Marekani, amesema: Wademocrat walioshinda katika uchaguzi inawapasa wajue kwamba, wamechaguliwa ili kufanya kazi kwa ajili ya Wamarekani, si kwa ajili ya kuonyesha upinzani na kumuuzulu rais.

Nancy Pelosi

Hata hivyo ni jambo la kutarajia kuwa, katika miaka miwili ijayo ya urais wake, Trump atakumbana na mashinikizo makubwa na mbinyo mkali wa Wademocrat, ambao wanauchukulia ushindi huu wa mwaka 2018 kama ngazi ya kukwea kuelekea ushindi wa uchaguzi wa rais wa mwaka 2020 na kurudi tena Ikulu ya White House. Na hasa kwa kuzingatia kwamba, uchaguzi wa mwaka huu umezidi kupanua ufa wa jamii iliyopasuka na kugawanyika vipande viwili ya Marekani, mpaka kufika hadi ya baadhi ya wataalamu, kutabiri uwezekano wa nchi hiyo kutumbukia hata kwenye aina mpya ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.../