Matokeo ya uchaguzi wa Kongresi ni ishara ya mgawanyiko mkubwa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i49352-matokeo_ya_uchaguzi_wa_kongresi_ni_ishara_ya_mgawanyiko_mkubwa_marekani
Mkuu wa Baraza la Uhusiano wa Kigeni Marekani amesema matokeo ya uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani yameonyesha kuwepo mgawanyiko mkubwa na wa kina katika jamii ya Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 07, 2018 13:04 UTC
  • Matokeo ya uchaguzi wa Kongresi ni ishara ya mgawanyiko mkubwa Marekani

Mkuu wa Baraza la Uhusiano wa Kigeni Marekani amesema matokeo ya uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani yameonyesha kuwepo mgawanyiko mkubwa na wa kina katika jamii ya Marekani.

Richard Haass amesema: "Matokeo ya uchaguzi wa katikati ya muhula Marekani yameonyesha kuwapo changamoto kubwa ndani ya nchi hii." Amebainisha kuwa pande mbili zinazohasimiana kisiasa yaani Wademokrat na Warepublican hawataweza kuafikiana na yamkini Trump akaelekeza nguvu zake katika masuala ya sera za kigeni.

Mchambuzi huyo wa siasa za Marekani ameongeza kuwa,  pande zote mbili hasimu zitajaribu kutumia matokeo ya uchaguzi wa Novemba 6 kwa maslahi yao katika uchaguzi wa rais utakaofanyika mwaka 2020.

Katika matokeo ya uchaguzi mdogo wa bunge la kongresi uliofanyika jana, Wademokrat wamechukua udhibiti wa baraza la wawakilishi huku Warepublikan wakiongeza nguvu yao katika udhibiti wa baraza la seneti katika bunge hilo la Marekani.

Bunge la Kongresi Marekani

Wademokrat  wanaelekea  kupata wingi wa viti katika baraza la wawakilishi ambavyo vilikuwa vinashikiliwa na Warepublikan. Matokeo ya hivi punde yanasema Wademokrat wana viti 222 katika baraza lenye wajumbe 435 ambapo kwa mujibu wa sheria wanahitaji viti 218 kulidhibiti bunge hilo.

Katika baraza la seneti, hadi sasa Warepublikan wamepata viti 51 na Wademocrat viti 45 katika baraza hilo lenye viti 100.