Amnesty: Saudia inawatesa wanaharakati kwa kuwabaka, kuwapiga kwa umeme
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limefichua kuwa, wapinzani na wanaharakati wa kisiasa nchini Saudi Arabia wanafanyiwa kila aina ya utesaji na udhalilishaji, ukiwemo udhalilishaji wa kingono, kupigwa kwa umeme na hata kupigwa mijeledi.
Amnesty International imesema ushahidi wa wahanga watatu wa jinai hizo umebainisha kuwa, mateso hayo ya kuogofya yamewafanya baadhi ya waathiriwa hao washindwe hata kusimama au kutembea.
Shirika hilo la msamaha duniani limesema kuwa, katika tukio moja, mwanamke aliyekuwa kizuizini nchini humo alibakwa na watu waliokuwa wamefunika nyuso zao wakati wa kusailiwa, huku mtetezi mmoja wa haki za binadamu wa jinsia ya kiume akifungwa miguu kwenye paa la jela na kuning'inizwa kichwa chini, miguu juu.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa shirika hilo lenye makao yake mjini London, aghalabu ya raia wa Saudia wanaoandamwa na mateso hayo ni wanazuoni na mawakili, na kwamba wengi wao huachiwa huru wakiwa wamelemaa tayari.
Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za wafungwa la Prisoners of Conscience la Saudia, watawala wa Riyadh wanawazuilia wanaharakati zaidi ya 2,500 wa upinzani, wakiwemo wanazuoni wa Kiislamu na waandishi wa habari.
Shirika hilo limesema kukamatwa, kuzuiliwa na kuteswa wanaharakati wa kisiasa nchini humo ni sehemu ya mbinyo na ukandamizaji unaofanywa na watawala wa Riyadh wakiongozwa na Mrithi wa Kiti cha Ufalme, Mohammed bin Salman kwa muda sasa.