Trump ana wasiwasi wa kuuliwa na askari wa Marekani walioko vitani
Gazeti moja la nchini Uingereza limeandika sababu ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kukataa kuwatembelea askari wa nchi hiyo walioko katika maeneo tofauti yenye vita duniani, ni wasiwasi wake wa kuogopa kuuliwa na askari hao.
The Independent limemnukuu kiongozi mmoja wa Marekani ambaye hakutaka kutaja jina lake akimsimulia mwandishi wa habari wa gazeti la Washington Post kwamba, Trump hawaamini wanajeshi wa Marekani walioko vitani na ana wasiwasi wasije wakamuua ndio maana anakataa kuwatembelea askari wa nchi yake katika maeneo tofauti ya vita duniani ikiwemo Iraq na Afghanistan, na kwamba wasiwasi huo amewaeleza hata watu wake wa karibu. Afisa huyo ameongeza kwamba kamwe rais huyo wa Marekani hataki kuzuru maeneo hayo na ana wasiwasi wa kuuliwa na askari hao wa nchi yake. Katika mazungumzo yake na vyombo vya habari Trump alidai kwamba sababu ya yeye kutowatembelea askari wa nchi yake huko Iraq na Afghanistan inatokana na kukosa muda, ingawa wakosoaji wake walikadhibisha madai hayo hasa kutokana na rais huyo kufanya safari za kila mara katika maeneo yake ya starehe.
Kadhalika Trump alisema uongo kwamba hakuunga mkono uvamizi wa nchi yake dhidi ya Iraq, katika hali ambayo mwaka 2003 rais huyo aliunga mkono uvamizi huo. Uvamizi wa Marekani wa mwaka 2001 nchini Afghanistan na kadhalika vita vyake nchini Iraq hapo mwaka 2003, mbali na kupelekea kuongezeka sana ukosefu wa amani ndani ya nchi hizo na eneo zima la Mashariki ya Kati, umeisababishia hasara kubwa pia Marekani hadi sasa.