Pompeo atiwa kiwewe na nafasi ya Iran ya kuwaunganisha Waislamu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ameonesha kughadhabishwa na matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba taifa hili linanyoosha mkono wa udugu kwa Waislamu wote duniani.
Mike Pompeo amesema matamshi ya Rouhani huenda yakachochea taharuki katika eneo la Mashariki ya Kati, na kwamba Iran sio rafiki wa Israel wala Marekani.
Katika taarifa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema, "Kwa mara nyingine tena Rais Rouhani wa Iran ametoa mwito wa kusambaratishwa Israel. Ameitaja Israel kuwa ni saratani na utawala bandia. Matamshi hayo yanaweza kuchochea taharuki katika eneo."
Akihutubia mkutano wa kila mwaka wa Umoja wa Kiislamu hapa Tehran, Rais Rouhani alisema, Waislamu hawana njia nyingine isipokuwa kuungana na kuwa kitu kimoja kwa ajili ya kupata ushindi dhidi ya Marekani na ubeberu wake.
Kadhalika alisema Iran inaiona Saudi Arabia kuwa ni ndugu yake na iko tayari kushirikiana na nchi hiyo kutatua matatizo yaliyopo.
Rais wa Iran aliyakosoa madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani na Uingereza, kwa kubuni haki ya turufu (veto) na kisha kuitumia haki hiyo kuunda donda la saratani katika eneo, linalofahamika kama utawala bandia wa Israel.