Onyo la Russia kwa chokochoko za Israel dhidi ya Syria
Balozi wa Russia mjini Beirut ameuonya vikali utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya kuendelea kuishambulia Syria kwa kutumia visingizio mbalimbali.
Katika mahojiano na gazeti la Lebanon la al-Akhbar leo Jumatatu, Alexander Zasypkin sambamba na kulaani chochoko hizo za Israel amesema utawala huo haramu unafanya hujuma dhidi ya Syria kwa madai ya kukabiliana na magenge ya kigaidi na uwepo wa Iran katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Amesema Russia na Iran zinashirikiana kwa karibu kulinda uhuru wa kujitawala Syria, mbali na kukabiliana na magenge ya kigaidi yanayotaka kuiangusha serikali halali ya Rais Bashar al-Assad.
Kadhalika mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Russia amezitaka nchi za Kiarabu zihuishe uhusiano wao na Syria pasina masharti yoyote, sambamba na kulisaidia taifa hilo kujijenga upya baada ya kushuhudia umwagikaji damu na uharibifu wa miundombinu tokea mwaka 2011.
Kauli ya balozi huyo wa Russia imekuja siku chache baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kufanya mashambulizi ya makombora ukilenga mji mkuu wa Syria, Damascus.
Hata hivyo mfumo wa ulinzi wa anga wa Syria ulitungua makombora hayo ya Israel, yaliyovurumishwa kutoka eneo la Galilee kulenga Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Damascus.