Majimbo 16 ya Marekani yafungua mashtaka dhidi ya Trump
https://parstoday.ir/sw/news/world-i51661-majimbo_16_ya_marekani_yafungua_mashtaka_dhidi_ya_trump
Majimbo 16 ya Marekani yamefungua mashtaka mahakama dhidi ya Rais Donald Trump wa nchi hiyo kufuatia hatua yake ya kutangaza hali ya hatari nchini humo kwa ajili ya kupata fedha za kujenga ukuta katika mpaka wa nchi hiyo na Mexico, suala ambalo limepingwa na Kongresi ya Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 19, 2019 12:16 UTC
  • Majimbo 16 ya Marekani yafungua mashtaka dhidi ya Trump

Majimbo 16 ya Marekani yamefungua mashtaka mahakama dhidi ya Rais Donald Trump wa nchi hiyo kufuatia hatua yake ya kutangaza hali ya hatari nchini humo kwa ajili ya kupata fedha za kujenga ukuta katika mpaka wa nchi hiyo na Mexico, suala ambalo limepingwa na Kongresi ya Marekani.

Mashtaka hayo yamewasilishwa katika mahakama ya jimbo la California ambayo iliwahi kutoa hukumu dhidi ya maamuzi ya Trump. Mashtaka hayo yametaja hatua ya Trump ya kutangaza hali ya hatari kwa ajili ya kupata fedha za kujenga ukuta huo kuwa ni kufanya udanganyifu na hila dhidi ya maamuzi ya Kongresi yanayohusiana na bajeti ya nchi.

Miongoni mwa majimbo yaliyowasilisha mashtaka hayo ni pamoja na Virginia, Maryland, New Jersey, New York, Delaware, Michigan na Minnesota.

Ijumaa iliyopita Donald Trump alitia saini tangazo la hali ya hatari kwa ajili ya kudhamini bajeti ya dola bilioni nane za kujenga ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico, suala ambalo limetajwa na viongozi wa chama cha upinzani cha Democratic kuwa ni "mapinduzi makubwa" dhidi ya katiba ya Marekani.

Spika wa Kongresi ya Marekani, Nancy Pelosi amesema kuwa, uamuzi huo unaokiuka sheria wa Trump ni mapinduzi makali dhidi ya Katiba na kwamba unaiteteresha Marekani kwa kuiba bajeti ya ulinzi.

Nancy Pelosi

Wakati huo huo maelfu ya watu wamefanya maandamano mbele ya Ikulu ya Rais wa Marekani, White House na katika makumi ya miji ya nchi hiyo wakipinga uamuzi wa Donald Trump wa kutangaza hali ya hatari kwa ajili ya kudhamini bajeti ya ukuta katika mpaka wa nchi hiyo na Mexico.