India yaituhumu Pakistan kwa kuhusika na shambulizi la Kashmir
Kamanda wa jeshi la India katika eneo la Kashmir Luteni Jenerali G S Dhillon amesema kuwa shirika la ujasusi la Pakistan limehusika katika hujuma iliyolenga msafara wa askari usalama wa nchi hiyo wiki iliyopita ambayo imeua zaidi ya askari 40 wa India.
Luteni Jenerali Dhillon amesema kuwa, jeshi la India lilimfuatilia mtu aliyetekeleza shambulizi hilo na kupata habari kwamba alikuwa akiongozwa na kupewa maelekezo kutoka nje ya mipaka kutoka kwa shirika la ujasusi la Pakistan.
Kamanda huyo wa jeshi la India katika jimbo linalogombaniwa la Kashmir ameongeza kuwa, hawezi kutoka taarifa zaidi kuhusu uchunguzi wa shambulizi hilo na nafasi ya shirika la ujasusi la Pakistan lakini amedai kuwa, kuna mfungamano mkubwa baina ya shirika hilo na makundi yenye misimamo mikali.
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Pakistan, Imran Khan ametoa pendekezo la kuishirikisha India katika uchunguzi juu ya shambulizi lililolenga msafara wa jeshi la nchi hiyo katika eneo la Pulwama kwenye eneo la Kashmiri linalodhibitiwa na India.
Imran Khan amesema kuwa, Pakistan iko tayari kupokea ripoti za kiintelijensia kutoka kwa India na kuzifanyia kazi. Hata hivyo amesisitiza kuwa, Pakistan itajibu hujuma na mashambulizi ya aina yoyote yatakayofanywa na India dhidi ya nchi hiyo baada ya mauaji ya Kashmir.
Alkhamisi iliyopita zaidi ya askari usalama 40 wa India waliuawa katika shambulizi la gari lililokuwa limetegwa mabomu katika eneo linalodhibitiwa na India la Kashmir.