Marekani inaipa Saudia teknolojia ya silaha za nyuklia
Ripoti ya Bunge la Kongresi nchini Marekani imebaini kuwa utawala wa Donald Trump uko mbioni kuikabidhi Saudi Arabia teknolojia ya siri ya kuunda silaha za nyuklia.
Ripoti ya Kongresi iliyotangazwa Jumanne imeonyesha kuwa, Rais Trump wa Marekani anahusika moja kwa moja katika jitihada za kuyawezesha mashirika ya Marekani ijenge vituo vya kuzalisha umeme wa nyuklia Saudi Arabia na kwamba teknolojia hiyo inaweza kutumika kuunda silaha za nyuklia.
Taarifa zilizofichuka zinaonyesha mawasiliano baina ya wakuu wa utawala wa Trump na mashirika ya nishati ya nyuklia nchini humo kuhusiana na kadhia hiyo ya kuipa Saudia teknolojia ya nyuklia.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa, wataalamu wana wasiwasi kuwa teknolojia nyeti ya nyuklia ya Marekani ikiwa mikononi mwa Saudia inaweza kutumiwa na ufalme huo kuunda silaha za nyuklia na hivyo kuhatarisha usalama wa Mashariki ya Kati.
Kongres imesema imeanzisha uchunguzi kuhusu hatua ya Trump kuiuzuia Saudia siri za kinyuklia za Marekani.
Mrithi wa ufalme wa Saudia Mohammad bin Salman mwaka jana aliweka msingi wa kituo cha kwanza cha utafiti wa nyuklia nchini humo mwezi Novemba mwaka jana. Saudia imekataa kutia saini sheria za kuizuia kutumia teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya kijeshi.