Pakistan yatimua nyambizi za jeshi la India, hali ingali tete
Pakistan inasema imeitimua kwa mafanikio nyambizi ya Jeshi la Majini la India ambayo ilijaribu kuingia katika mipaka yake ya baharini huku hali ikiwa bado ni tete baina ya madola hayo jirani yanayohasimiana na ambayo yana silaha za nyuklia.
Katika taarifa siku ya Jumanne, Jeshi al Majini la Pakistan limesema lilitumia mbinu maalumu kuitimua nyambizi hiyo ya India na kuizuia kuingia katika maji ya Pakistan Jumatatu usiku.
Taarifa hiyo imesema oparesheni hiyo ni dhihirisho kuwa Jeshi la Majini la Pakistan lina uwezo mkubwa na kwamba jeshi hilo litaendelea kulinda mipaka ya majini na kukabiliana na hujuma yoyote ile.
Jeshi la Majini la Pakistan limesema lilijizuia kuihujumu nyambizi hiyo ya India kutokana na sera za serikali ya Waziri Mkuu Imran Khan ambaye amesisitiza kuhusu kudumisha amani.
Katika tukio jingine, vyombo vya habari vya India vimesema ndege ya kivita ya India aina ya Sukhoi-30 imeitungua ndege isiyo na rubani ya Pakistan (drone) katika jimbo la kaskazini mwa India la Rajasthan Jumatatu.
Matukio hayo mawili ni msururu wa oparesheni za kijeshi baina ya India na Pakistan zilizoanza wiki iliyopita wakati India iliposhambulia ngome ya kundi la kigaidi la JeM ndani ya ardhi ya Pakistan. India ilisema kundi hilo lilihusika katika hujuma dhidi ya askari wake katika eneo la Kashmir linalotawaliwa na India mnamo Februari 14. Katika tukio hilo askari zaidi ya 40 wa India waliuawa. Pakistan ilijibu mapigo Jumatano iliyopita kwa kutungua ndege mbili za kivita za India na kumteka rubani ambaye aliachiliwa baada ya siku mbili katika hatua ambayo wakuu wa Pakistan waliitaja kuwa ni ya kutuliza hali ya mambo na kurejesa amani.
India na Pakistan zimekuwa zikizozana kwa muda mrefu kuhusu eneo la Jamu na Kashmir na zimepigana vita mara tatu kuhusu eneo hilo.