Trump awashambulia Wademocrati, asema ni vichaa na majnuni
Rais Donald Trump wa Marekani amewatuhumu viongozi wa chama cha upinzani cha Democratic kuwa ni wendawazimu na kwamba wanambughudhi.
Trump amesema hayo kufuatia uchunguzi unaofanywa na Tume ya Masuala Mahakama ya Kongresi ya nchi hiyo kuhusu ufisadi na uhalifu uliofanywa na kiongozi huyo.
Trump anayeandamwa na tuhuma za kushirikiana na Russia katika uchaguzi uliopita wa Rais wa Marekani ameendelea kumtuhumu aliyekuwa mpinzani wake katika uchaguzi huo, Hillary Clinton akisema yeye na Wademocrati wenzake ndio walioshirikiana na Russia na kusema Mwenyekiti wa Kamati ya Mahakama ya Kongresi, Jerry Nadler na Mwenyekiti wa Tume ya Upelelezi, Adam Schiff na viongozi wa chama cha Democratic wamepatwa na kichaa.
Wakati huo huo ikulu ya Rais wa Marekani White House imewashambulia vikali viongozi wa chama cha Democratic ikisema uchunguzi unaofanyika kuhusu tuhuma za uhalifu wa Donald Trump umechochewa na wale walioanzisha kampeni ya kutaka kumuuzulu.
Mivutano ya kisiasa imepamba moto nchini Marekani baada ya chama cha Democratic kushinda uchaguzi wa katikati ya msimu Novemba mwaka uliopita.
Miongoni mwa masuala mengine yatakayopewa mazingatio na kumulikwa zaidi na Bunge jipya la Marekani ni kutazama umpa siasa za serikali ya Trump na uhusiano wake utawala wa Saudi Arabia.
Vilevile Kamati ya Uhusiano wa Nje ya Kongresi itachunguza kwa makini jinsi White House ilivyoshughulikia kadhia ya mauaji ya mwandishi na mkosoaji wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi katika ubalozi wa mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul.
Donald Trump na maafisa wa serikali yake wameendelea kuikingia kifua Saudi Arabia licha ya hata shirika la ujasusi la nchi hiyo CIA kuthibitisha kwamba, Jamal Khashoggi aliuawa kwa amri ya Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman.